TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA AALCO
Na Mwandishi Wetu, Kampala - Uganda. TANZANIA ni mwanachama wa AALCO, imeshiriki katika Mkutano wa 63 uliofanyika Kampala, Uganda, ambapo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Bibiana Kileo, na TAKUKURU ikiwakilishwa na Mchunguzi Kiongozi Msaidizi Debora Elisha Mlowe kutoka Kurugenzi ya Huduma za Sheria. Ushiriki huu unaonesha nafasi muhimu ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa na urejeshaji wa mali zinazopatikana kutokana na vitendo vya rushwa. Katika mkutano huo wa siku tano, Tanzania imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na makosa ya kimataifa yanayovuka mipaka, pia imeunga mkono juhudi za kuimarisha nyanja za urejeshaji wa mali na utaifishaji mali, hatua inayodhihirisha dhamira ya taifa katika kulinda rasilimali na kuimarisha uwajibikaji barani Afrika na Asia.