MTANDAOO WA MSHIKAMANO WA KIMATAIFA UMEANDAA SALUNI YA KITAMADUNI KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA MSHIKAMANO WA KUSINI MWA DUNIA.

 














*"Mazungumzo ya Mshikamano wa Kimataifa" huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Kusini mwa Dunia*

Na Mwandishi Wetu, Egypt 

KATIKA  kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano wa Kusini, Mpango wa Mazungumzo ya Mshikamano wa Kimataifa unaosimamiwa na Mtandao wa Mshikamano wa Kimataifa umeanda saluni ya kitamaduni. 

Saluni hiyo yenye mada: "Vyama vya Ushirika katika Kusini ya Duniani", sambamba na tamko la Umoja wa Mataifa la kutangaza mwaka 2025 kuwa mwaka wa vyama vya ushirika chini ya kauli mbiu: "Vyama vya Ushirika: Sauti ya Pamoja ya Kusini Duniani kuelekea Mustakabali Endelevu."

Saluni hiyo imemkaribisha Dkt. Mohamed Abdel Hakim Ibrahim, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Uchumi wa Kijamii na Ushirika katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, na mwandishi wa kitabu cha “Vyama vya Ushirika na Maswali ya Maendeleo”, kama mzungumzaji mkuu katika Saluni hiyo. 

Pia Saluni hiyo ilihudhuriwa na Mtafiti Hassan Ghazaly, Mwanzilishi wa Mtandao wa Mshikamano wa Kimataifa, na Dkt. Sally Saad, Mtaalamu na Mshauri wa Kimataifa wa Mawasiliano na Mahusiano ya Umma, na mhadhiri wa Mahusiano ya Umma katika Taasisi Kuu ya Al Jazeera ya Vyombo vya Habari na Mawasiliano, waliokuwa wachambuzi. 

Kikao hiki kimeongozwa na Dkt. Mohamed Sayaf, Mhadhiri msaidizi (Mtafiti Mwandamizi) katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi wa Kilimo na Kituo cha Utafiti wa Kilimo.

Ushirika: Kuushirikisha Ubinadamu katika Sayansi ya Uchumi. 

Dkt. Mohamed Abdel Hakim Ibrahim ameanza hotuba yake katika saluni ya “Ushirika katika Kusini mwa Dunia” kwa kuuliza washiriki: “Kwa nini tunahitaji vyama vya ushirika? Na ni aina gani ya ushirika tunaouhitaji?” Akasisitiza kwamba kazi yoyote ya maendeleo haipaswi kuishia kwenye vipengele vya kiuchumi vinavyohusiana na faida na ukuaji pekee, bali inapaswa kuvuka mipaka hiyo na kujumuisha maendeleo ya kitamaduni, kielimu na kisayansi, sambamba na umuhimu wa kutofautisha kati ya ukuaji wa uchumi na maendeleo jumuishi.

Katika muktadha huo, Abdel Hakim alichambua dhana ya uchumi wa kijamii na ushirika, akiieleza kama jaribio la kujibu swali kuu: “Je, inawezekana kuwepo uchumi unaomgusa zaidi mwanadamu?” Hii ndiyo fikra aliyoitaja mchumi Samir Amin kwa jina la “kuushirikisha ubinadamu katika sayansi ya uchumi”.

Alifafanua kwamba uchumi wa kijamii na ushirika ni mtazamo unaolenga kukidhi mahitaji ya kibinadamu, kijamii na kimazingira, badala ya kutafuta faida ya juu zaidi, Unajengwa juu ya misingi ya mshikamano, uwajibikaji wa pamoja, na utawala wa kidemokrasia. 

Uchumi huu huchukua sura mbalimbali, ikiwemo:

• Vyama vya ushirika wa kilimo, ushirika wa wafanyakazi na ushirika wa makazi.

• Mashirika ya misaada na taasisi zisizo za kibiashara.

• Makampuni ya kijamii.

Aidha, alisisitiza kwamba utekelezaji wa mfano huu unahitaji hatua na mikakati jumuishi katika ngazi za kisiasa, kisheria na kijamii. Akabainisha kwamba uchumi wa kijamii na ushirika unaweza kuwa injini kuu ya maendeleo endelevu, uundaji wa ajira, kuboresha viwango vya maisha, na kupunguza tofauti za kijamii.

Ushirika: Mwitikio wa Kibinadamu kwa Changamoto za Mapinduzi ya Viwanda

Dkt. Abdel Hakim akielezea historia ya kuzaliwa kwa harakati za ushirika duniani, amesisitiza kuwa halikuwa tu wazo la kiuchumi, bali lilijitokeza kama mwitikio wa kibinadamu kwa changamoto zilizotokana na Mapinduzi ya Viwanda barani Ulaya.

Amefafanua zaidi kuwa uhamaji wa jamii kutoka vijijini kwenda mijini, pamoja na ukuaji wa mfumo wa kibepari uliowekwa juu ya faida bila kuzingatia vipengele vya kijamii, uliibua pengo kubwa kati ya wamiliki wa mitaji na wafanyakazi.

Ameongeza kuwa uchumi wa kibepari kwa wakati huo ulishindwa kupokea idadi kubwa ya wafanyakazi, jambo lililosababisha kuenea kwa umasikini, unyonyaji na kudorora kwa hali ya maisha, hapo ndipo ikajitokeza haja ya kuwa na mbadala wa kiuchumi unaomweka binadamu katikati ya malengo yake. 

Hivyo ukaibuka ushirika ulioweka misingi na thamani madhubuti ikiwemo uanachama wa wazi na wa hiari, usimamizi wa kidemokrasia, ushiriki wa kiuchumi wa wanachama, uhuru na kujitegemea, elimu na mafunzo, ushirikiano kati ya vyama vya ushirika, pamoja na kujali jamii. 

Kwa misingi hii haikuwa kauli mbiu tu, bali iliunda ramani ya njia ya kuanzisha taasisi za kiuchumi zenye uwezo wa kuwahudumia wanachama wake na jamii zao kwa njia endelevu.

Aidha, Dkt. Abdel Hakim aligusia aina za umiliki, akibainisha kuwa vyama vya ushirika vinawakilisha mfano wa kipekee wa umiliki wa pamoja, tofauti na umiliki wa umma (wa serikali) na umiliki binafsi (wa mtu mmoja).

Katika muktadha huu, alieleza baadhi ya uzoefu wa ndani nchini Misri katika vyama vya ushirika wa kilimo, vimevyoonesha mafanikio katika kuboresha maisha ya wakulima na kuongeza tija yao.

Ushirika: Nguvu Inayoendesha Maendeleo

Kwa upande wake, Dkt. Mohamed Sayaf, Profesa Msaidizi (Mtafiti Mwandamizi) katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi wa Kilimo na Kituo cha Utafiti wa Kilimo, na Mratibu wa Shule ya Mshikamano wa Kusini Duniani, katika hotuba yake amesisitiza umuhimu mkubwa wa vyama vya ushirika vya kiuchumi na kijamii, akibainisha aina zake mbalimbali nchini Misri. 

Hata hivyo, ameeleza kwamba vyama vya ushirika wa kilimo peke yake vimenufaisha takribani watu milioni 12.5, sambamba na vyama vya ushirika vya ufundi, vya walaji na vinginevyo.

Sayyaf alipanua mazungumzo yake kujumuisha pia uzoefu wa kimataifa katika nchi za Kusini Duniani, akisisitiza kwamba nyingi kati ya nchi hizo ziliiga uzoefu wa Misri katika miaka ya sitini, hususan nchi za zisizofungamana na upande wowote ambazo zilijitahidi kujiondoa kwenye mfumo wa kibepari wa kikoloni. 

Katika muktadha huu, ametaja mfano wa Tanzania mwishoni mwa miaka ya sitini na mwanzoni mwa miaka ya sabini, ambapo kulitokea hatua kubwa ya kimaendeleo kutokana na utegemezi wake kwa vyama vya ushirika. Wakati huohuo, alielekeza pia kwenye juhudi za Rais Abdel Fattah El-Sisi kuhusu sheria za ushirika na mbinu za kuviunda, akifafanua kwamba dhamana ya kweli ya kudumu kwa miradi inayohudumia sekta 23 tofauti ni uwepo wa vyama vya ushirika imara na vinavyofanya kazi kwa ufanisi.

Ushirika wa Habari: Sauti ya Pamoja kwa Kusini Duniani

Katika maoni yake, Dkt. Sally Saad alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa kile alichokiita “ushirika wa habari” kati ya nchi za Kusini Duniani, na akavielezea kama “sauti ya pamoja ya Kusini Duniani”, kwa kuwa ni chombo cha kuziba pengo la habari na kuimarisha uwepo wa masuala ya Kusini katika mazingira ya mwingiliano wa kimataifa unaoharakishwa.

Dkt. Sally alieleza kwamba vyama hivi vya ushirika vinatoa fursa ya kuzalisha maudhui halisi na ya kuaminika yanayoakisi masuala ya jamii za wenyeji bila upotoshaji, na pia hutoa jukwaa la kubadilishana uzoefu na maarifa kati ya wanahabari, pamoja na kuunganisha rasilimali ili kuimarisha uwezo wa pamoja wa habari. Pia alibainisha changamoto kuu zinazolikabili mfano huu katika nchi za Kusini Duniani, ikiwemo: pengo la habari na kutopewa nafasi kwa baadhi ya masuala, udominishaji wa ajenda za kigeni, upungufu wa rasilimali, na changamoto za kiteknolojia.

Amehitimisha hotuba yake kwa kuwasilisha uzoefu wa “Mtandao wa Wanahabari wa Tabianchi Afrika” (ACJN), akiuonesha kama mfano uliofanikiwa wa ushirikiano wa kikanda wa habari katika uwanja wa masuala ya tabianchi, akisisitiza kwamba kuanzishwa kwa vyama vya ushirika vya aina hii ni hatua ya kimkakati ya kurejesha udhibiti wa simulizi za habari na kuimarisha uwepo wa nchi za Kusini katika medani ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mtafiti Hassan Ghazaly amesisitiza kwamba Mtandao wa Mshikamano wa Kimataifa ni mwavuli unaokusanya miradi kadhaa iliyoanzishwa kwa namna ya hatua kwa hatua tangu mwaka 2012, yenye lengo la kukuza roho ya kufanya kazi kwa pamoja na kuimarisha thamani za mshikamano kwa sura zake mbalimbali. Alieleza kwamba miongoni mwa miradi maarufu inayoakisi upeo wa shughuli na dira yake yenye lengo la kuimarisha mazungumzo na mawasiliano ni: Fomu ya Uigaji wa Umoja wa Afrika, Mpango wa Afrimedia, Mradi wa Bozoor kwa ajili ya utamaduni wa umma, Shule ya Mshikamano wa Kusini Duniani, Mradi wa kitaifa wa uelimishaji kuhusu Mkataba wa Biashara Huru ya Afrika, Mradi wa Mshikamano wa Watu wa Bonde la Nile, na Mpango wa Mazungumzo ya Mshikamano wa Kimataifa.

Ni vyema kutajwa kuwa saluni hiyo ilishuhudia ushiriki mkubwa kutoka kwa hadhira waliotoa michango na maswali mbalimbali, wakionesha uzoefu wa ushirikiano kutoka nchi za Kusini Duniani kama vile China. 

Shughuli hizo zimehitimishwa kwa mtafiti Hassan Ghazaly kumtunuku Dkt. Mohamed Abdel Hakim Ibrahim zawadi ya heshima na kwa kupigwa picha za pamoja za kumbukumbu.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.