SERIKALI YASHAURIWA KUVIPA RUZUKU VYOMBO VYA HABARI
Na Mwamdishi Wetu, WAHARIRI nchini, wameishauri serikali kuvipa ruzuku Vyombo vya Habari ili vifanye kazi kwa ufanisi zaidi. Akizungumza kwenye semina ya siku moja iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) leo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alitoa kauli hiyo iliyoungwa mkono na Wahariri wenzake. “Hatuwezi kufanya kazi vizuri bila kuwezeshwa, tuachane na kutoka mataifa ya nje kwamba, serikali ikiwezesha Vyombo vya Habari, havitakuwa huru. “Tunaonaje aibu kuviwezesha Vyombo vya Habari ili vijenge miundombinu ya fikra ili watu wasichome nchi yao? Mbona Vyama vya Upinzani vinapewa ruzuku na bado vinaisimamia serikali bila kuyumbishwa?” amesema Balile. Balile alitoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Hamis Masauni kushauri Vyombo vya Habari kuelimisha wananchi hususani vijana kuhusu faida na fursa zilizopo ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.