COSTECH YAJENGA KITOVU CHA TAASISI ZA UBUNIFU NA UTAFITI DODOMA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma TUME ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) inatekeleza kwa kasi mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Makao Makuu mapya jijini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuiweka Tanzania kwenye msitari wa mbele katika maendeleo ya maarifa, utafiti na ubunifu wa kisayansi. Ujenzi huo, unaotarajiwa kukamilika Machi 2026, umeelezewa na viongozi wa COSTECH kuwa ni zaidi ya jengo bali ni uwekezaji wa taifa katika mustakabali wa uchumi wa ubunifu na teknolojia ya kisasa. Kwa mujibu wa Dkt. Amos Nungu, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, jengo hilo litakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa watafiti, wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia kwa kutumia miundombinu ya kisasa ikiwemo maabara bunifu, vituo vya Atamizi, kumbi za mikutano ya wataalamu, na ofisi zilizounganishwa na mifumo ya kidigitali. “Tunajenga jukwaa la kisayansi litakalosaidia taifa kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi, tafiti, na maarifa. Dodoma sasa inapata nafasi ya kuwa moyo wa uvumbuzi nchini,” alisema Dkt. Nungu. Nay...