WAKUU WA IDARA NA VITENGO IGUNGA WAGAWIWA VISHIKWAMBI ILI KUACHANA NA MATUMIZI YA KARATASI.
Na Mwandishi Wetu, Igunga. WAKUU wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wamegawiwa Vishikwambi kwa lengo la kuvitumia katika vikao mbalimbali na kuachana na matumizi ya karatasi. Akizungumza baada ya kuwagawia vishikwambi hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Hamid amesema wanaendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika matumizi ya kidijitali. Amesema hatua hiyo, inaendelea kuondoa mnyororo wa matumizi ya karatasi ambazo hutengenezwa kwa miti, hivyo kuendelea kutunza miti kwa mazigira rafiki kwa mwanadamu. Aidha, amewataka wakuu hao wa Idara na Vitengo kuvitumia vishikwambi hivyo kuongeza ufanisi wa kazi huku akiwasihi kutojaza picha na taarifa zisizohusiana na Menejimenti.