CHUO CHA UHASIBU ARUSHA MABINGWA SHIMIVUTA
Na Allan Kitwe, Tabora
CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA) kimetwaa ubingwa wa jumla wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (SHIMIVUTA) yaliyomalizika jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora.
IAA imetwaa ubingwa huo baada ya kushika nafasi ya kwanza kati ya vyuo vikuu 16 vilivyoshiriki mashindano hayo mwaka huu kati ya Vyuo Vikuu 25 wanachama wa Shirikisho hilo.
Chuo hicho kimekuwa mshindi wa kwanza katika mchezo wa riadha, draft, bao, mpira wa mikono, wavu na kushika nafasi ya pili katika michezo ya pool table, pete, kikapu na nafasi ya tatu kwenye karata.
Rais wa Shirikisho hilo Juhudi Elirehema Sam ameeleza kufurahishwa na mashindao ya mwaka huu kutokana na ushindani mkubwa ulikuwepo na kuahidi kuwa mwakani maandalizi yatakuwa makubwa zaidi ya hapo.
Amesistiza kuwa licha ya viwanja kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini timu zote zilicheza kwa ustadi mkubwa na kuonesha vipaji vya hali ya juu.
Akihitimisha mashindano hayo jana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Dkt John Pima amewashukuru Wakuu wa Vyuo, waratibu na walimu kwa kufanyia mashindano hayo katika Mkoa huo mwaka huu.
Ameongeza kuwa yameleta neema kubwa kwa wakazi wa manispaa hiyo kupitia huduma mbalimbali walizokuwa wakitoa wakati wote wa mashindano hayo ikiwemo malazi, chakula, usafiri na mambo mengine mengi.
Ameahidi kuwa Mkoa kupitia manispaa hiyo watawapa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha mashindano ya mwakani yanakuwa na ushindani mkubwa zaidi na kuleta burudani ya kutosha kwa wakazi wa halmashauri hiyo na Mkoa mzima wa Tabora.





Maoni