WATAALAM WA MAABARA WATAKIWA KUSIMAMIA WELEDI NA MATUMIZI SAHIHI YA RASILIMALI
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam. Wataalam wa maabara wametakiwa kusimamia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali ili kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa jamii. Wito huo umetolewa leo, Desemba 19, 2025, na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya Bw. Issa Ng’imba wakati wa mahafali ya mafunzo ya Global Laboratory Leadership Program (GLLP) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Bw. Ng’imba amesema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo viongozi chipukizi wa maabara katika masuala ya uongozi na kuwapa mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi. Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, hasa katika kipindi ambacho kuna hitaji la kuimarisha mifumo ya maabara, hususan katika masuala ya utawala, utatuzi wa kero za wagonjwa, upimaji pamoja na ushiriki katika ufuatiliaji wa magonjwa. “Niishukuru Serikali pamoja na mdau wetu, Global Fund, kwa kutambua umuhimu wa ku...