TASAC YAKUSANYA MAONI YA MAREKEBISHO YA NAULI ZA MV. BIJLEE NA MV. NYEHUNGE
Na Lubango Mleka, Mwanza.
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 16 Desemba 2025 limefanya mkutano wa wadau jijini Mwanza kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu maombi ya marekebisho ya nauli za meli za MV. Bijlee na MV. Nyehunge, zinazofanya safari kati ya Mwanza na Nansio- Ukerewe katika Ziwa Victoria.
Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Dominic ulifunguliwa rasmi na Bw. Nahson Sigalla, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, waendeshaji wa meli, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri wa majini jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bw. Sigalla amesema kuwa maombi ya marekebisho ya nauli yamewasilishwa na Kampuni ya Manoj V. Mehta Investments Ltd., waendeshaji wa MV. Bijlee, na Said Mohamed & Brothers Co. Ltd., waendeshaji wa MV. Nyehunge.
Alieleza kuwa kikao hicho kimeandaliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, kinachotaka ushirikishwaji wa wadau kabla ya uridhiwaji wa tozo au marekebisho ya nauli.
“Zoezi hili linalenga kuhakikisha uwazi, ushirikishwaji mpana, na maslahi ya watumiaji wa huduma za usafiri wa majini yanazingatiwa ipasavyo kabla ya uamuzi wowote kufanyika. Na maoni yote yatakusanywa na kuzingatiwa kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho kuhusu idhini ya marekebisho ya nauli,” amesema Bw. Sigalla.
Katika mkutano huo, waendeshaji wa meli waliwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya nauli pamoja na sababu zilizochochea maombi hayo, huku wadau wakichangia kuhusu mapendekezo hayo na kutoa maoni yao.
TASAC imetoa wito kwa wadau ambao hawakupata nafasi ya kutoa maoni yao wakati wa mkutano kuwasilisha maoni kwa maandishi katika ofisi zake za Mwanza au Dar es Salaam kabla au ifikapo tarehe 30 Desemba 2025.










Maoni