DKT SEIF- TUREJESHE TABASAMU KWA WANANCHI KWA KUTOA HUDUMA BORA
Na Lubango Mleka, Mwanza.
VIONGOZI katika ngazi zote wametakiwa kuhakikisha wanarejesha tabasamu kwa watanzania kwa kuwapeleka huduma bora ikiwa ni sambamba na kusimamia na kutunza miundombinu iliyopo ili iweze kuleta tija na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Jafar Seif (MB) tarehe 16 Desemba, 2025 na) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Manispaa ya Ilemela ambapo lengo kuu la ziara ni kutembelea miradi ya afya pamoja na kukutana na watumishi kwa ajili ya kujadili na kubaini changamoto zinazoikablili sekta hiyo katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI ni jukumu letu kuhakikisha kwamba tunamsaidia Mhe. Rais kurudisha tabasamu kwa watanzania, ahadi ambayo aliitoa wakati akilihutubia bunge la 13 ambapo aliahidi kwamba ndani ya awamu ya sita kipindi cha pili tuhakikishe tunarejesha tabasamu kwa watanzania kwa kuwapeleka huduma bora ”amesema Dkt Jafar
Dkt. Jafar amefafanua kuwa huduma bora inatafsiriwa kuwa ni upatikanaji wa huduma za afya wa uhakika ikiwa ni sambamba na kujenga zahanati na vituo vya afya vya kisasa akitolea mfano ujenzi wa kituo cha afya Nyambiti kilichopo kata ya Buzuruga alichokitembelea wakati wa ziara yake.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Nyambiti, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt. Maria Kapinga amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutawawezesha zaidi ya wakazi 7,571 wa eneo hilo kupatiwa huduma na kupunguza msongamano katika kituo cha afya Buzuruga ambapo wananchi wa maeneo hayo hulazimika kwenda kupatiwa huduma.
Hadi kukamilika mradi utagharimu shilingi milioni 144.7 na unatarajiwa kukamilika pamoja na kuanza kutoa huduma mwezi Januari mwaka 2026.








Maoni