MWENYEKITI SIKONGE AHIMIZA KASI YA MAENDELEO

 













Na Allan Kitwe, Sikonge.

MWENYEKITI wa Halmasahauri ya Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Andrea Gasto amewataka Madiwani na Watendaji wa halmashauri hiyo kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya sita katika kukusanya mapato ili kuharakisha maendeleo.

Ametoa rai hiyo jana alipokuwa akiongea na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo baada ya kuchaguliwa kwa kishindo kuongoza halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, yaani 2025-2030.

Amesema kuwa wakazi wa Halmashauri hiyo wana imani na matumaini makubwa na madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo na wako tayari kuwapa ushirikiano ili kuchocheo kasi ya maendeleo yao.

Mwenyekiti amedokeza kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alishatoa mwelekeo wa yale atakayowafanyia wana Sikonge ndani ya siku 100 na mengineyo mengi kama yalivyobainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030.

‘Wakazi wa Sikonge wana imani kubwa na serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi, naomba kila mmoja aliyepewa dhamana ya kusimamia maendeleo yao afanye kazi kwa bidii na moyo wa dhati’, ameeleza.

Akitoa salamu za serikali katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya hiyo Thomas Myinga amewataka madiwani na wataalamu kuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi na kuwaeleza umuhimu wa miradi inayotekelezwa na serikali.

Amewataka kusimamia ipasavyo suala zima la ukusanyaji mapato katika maeneo yao ili kuongeza mapato ya halmashauri na kuchochea kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo ndani ya kata yake.

Aidha amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Seleman Pandawe kuhakikisha miradi ya nyuma yote inatengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu ili utekelezaji wake uendelee na kuwanufaisha watoto.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.