RAIS MWINYI:SMZ ITAENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA USAJILI KIDIJITALI.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar. RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usajili kidijitali wa matukio ya kijamii kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 10 Agosti, 2025 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usajili Barani Afrika yaliyofanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi. Ameeleza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi unaofanywa na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) katika usajili wa vizazi, vifo, talaka, ndoa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi. Rais Dkt. Mwinyi amesema hakuna maendeleo ya kweli bila usajili wa utambulisho wa wananchi katika mifumo imara inayotambulika kisheria na inayotumia teknolojia ya kisasa ya kidijitali. Aidha, Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa ZCSRA kuanzisha kampeni maalum kwa kushirikiana na masheha kuha...