WAZIRI MCHENGERWA AZITAKA TAASISI ZA AFYA KUJITATHMINI KUELEKEA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Na WAF, Dodoma. WAZIRI wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara ya Afya na Vituo vyote vya kutolea huduma kujitathmini utendaji kazi wake, mapungufu na changamoto na kuona namna gani ya kutatua changamoto hizo wakati Serikali ikielekea kwenye utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote. Waziri Mchengerwa amesema hayo Januari 14, 2026 jijini Dodoma katika kikao kazi kilichohusisha Wakurugenzi Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Watumishi wote wa Sekta ya Afya. Mhe. Mchengerwa amesema Bima ya Afya kwa Wote italeta ongezeko la matumizi ya huduma za afya hivyo amevitaka vituo vyote vya kutolea huduma za Afya kuanzia ngazi ya msingi mpaka Taifa kuimarisha huduma wanazo zitoa. “Wananchi waliokuwa wanajizuia kufika Hospitalini kwa sababu ya gharama sasa watafika. Huduma zitahitajika kwa wingi zaidi, kwa kasi zaidi, na kwa ubora unaofanana”, amesema Waziri Mchengerwa...