VIKUNDI 222 UYUI VYAWEZESHWA MIKOPO NAFUU YA BILIONI 1
Na Allan Kitwe, Tabora. HALMASHAURI ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora imetoa mikopo nafuu isiyo na riba ya shilingi bilioni 1 kwa vikundi 222 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo ili kuwainua kiuchumi. Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi za mikopo hiyo jana, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo Amoniche Mtweve amesema kuwa mikopo hiyo imetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Ameongeza kuwa jumla ya wanachama 1,121 wanaounda vikundi hivyo wamenufaika na mikopo hiyo na kuwapa nguvu ya kuendeleza miradi yao ya biashara na uzalishaji mali katika maeneo yao. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Shabani Katalambula, amewataka wanufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine kunufaika na mikopo hiyo katika awamu zijazo. Amefafanua lengo la mikopo hiyo kuwa ni kusaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kupitia miradi midogo midogo ya ujasiriam...