MADIWANI TABORA WAPEWA MAFUNZO YA UWAJIBIKAJI
Na Allan Kitwe, Tabora
MADIWANI wa halmashauri ya manispaa Tabora na Uyui Mkoani Tabora wamepewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni.
Akifungua mafunzo hayo leo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mohamed Katete amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ili kuwajengea uwezo.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa kuwa yatawaongezea weledi katika kusimamia utendaji wa halmashauri zao na kuongeza kasi ya kutumikia wananchi waliowachagua katika kata zao.
‘Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mafunzo haya yatolewe kwa madiwani wote nchini ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa weledi mkubwa na kukamilika kwa wakati’, ameeleza.
Aidha amewataka kujenga mahusiano mazuri na wataalamu na watendaji wa halmashauri zao na kuhakikisha fedha zinazoletwa na serikali kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo na zile za mapato ya ndani zinafanya kazi iliyokusudiwa.
Ametoa wito kwa madiwani wote kuzingatia malengo ya mafunzo hayo ili utendaji wao ulete tija kwa halmashauri zao na wananchi kwa ujumla.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Ghullam Hussein Dewj amempongeza Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo hayo kwa madiwani baada ya kuchaguliwa kwa kuwa utawaongezea ufanisi.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma ambao ndiyo waratibu wa mafunzo hayo, Mwezeshaji Ismail Juma Kaudunde amesema kuwa mafunzo hayo ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita kuwapa uwezo, mbinu na maarifa ya kusimamia utendaji wa halmashauri.
Ametaja sifa za Kiongozi bora kuwa ni yule anayetimiza wajibu wake kikamilifu kwa anawaongoza, muwazi, mwajibikaji, muadilifu, jasiri na anayeonesha njia sahihi.




Maoni