MAPATO MANISPAA YA TABORA YAPAA
Na Allan Kitwe, Tabora.
HALMASHAURI ya manispaa Tabora imeendelea kupiga hatua kubwa kimaendeleo ikiwemo kufanikisha utekelezaji miradi ya maendeleo kutokana na kasi nzuri ya ukusanyaji mapato kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt John Pima alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya rasimu ya bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika kikao cha Baraza la madiwani.
Amefafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wanatarajia kukusanya zaidi ya sh bilioni 12 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali ikiwa ni sehemu ya rasimu ya mapendekezo ya bajeti yao kwa mwaka huu wa fedha.
Amedokeza kuwa mapendekezo hayo ni ishara ya kazi nzuri ambayo imeendelea kufanywa na timu yake ya mapato kwa mwaka wa fedha uliopita ambapo walipanga kukusanya kiasi cha sh bilioni 8.6 na kupata mafanikio makubwa.
Dkt Pima amefafanua kuwa kati ya kiasi hicho sh bilioni 10.57 ni mapato halisi na kiasi cha sh bilioni 1.68 ni mapato fungwa yanayotokana na mafanikio makubwa waliyopata katika mwaka wa fedha uliopita, yaani 2025/2026.
Ametaja mambo yanayochochea ongezeko la mapato kuwa ni kuimarishwa usimamizi wa ukusanyaji kwa kila chanzo, kuanzishwa miradi mipya ikiwemo minada ya awali 3, ujenzi wa hosteli ya wanafunzi na kiwanda cha kufyatua tofali.
Mengine yanayochochea kupaa mapato ya manispaa hiyo alisema kuwa ni kuboreshwa miradi iliyopo katika maeneo mbalimbali kama vile masoko na vibanda vya biashara na mwenendo mzuri wa makusanyo kwa mwaka 2025/2026.
Dkt Pima amewasilisha mapendekezo ya mapato na matumizi ya kiasi cha sh bilioni 60.9 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo sh bil 34.5 ni ruzuku ya mishahara na sh bil 2.1 ruzuku ya matumizi ya kawaidi zote kutoka serikali kuu.
Shilingi bil 3.1 ni matumizi ya kawaida kutoka mapato ya ndani na bil 1.6 ni za mapato fungwa ya halmashauri, fedha za miradi ya maendeleo ni sh bil 18.8 ( bil 6.9 ni za mapato ya ndani, bil 7.7 serikali kuu na bil 4.1 ni za wahisani).
Amebainisha vipaumbele vya halmashauri hiyo kuwa ni kumalizia viporo vya miradi yote ili kuboresha utoaji huduma za kijamii, kiuchumi na utawala, kuboresha zoezi la ukusanyaji, kuanzisha miradi ya uwekezaji na kuboresha usafi.




Maoni