TANZANIA YANG'ARA DUNIANI KUNDI LA VINARA WA SERIKALI KIDIGITALI - WORLD BANK 2025.
Na Hamida Ramadhani. TANZANIA imeendelea kung’ara kimataifa baada ya Benki ya Dunia (World Bank – WB) kuitaja kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ukomavu wa juu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta ya umma. Hatua hii ni uthibitisho wa mafanikio ya mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kutekelezwa na Serikali katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Kwa mujibu wa Ripoti ya GovTech Maturity Index (GTMI) ya mwaka 2025, Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A – Ukomavu wa Juu wa Matumizi ya TEHAMA (Extensive GovTech Maturity). Kundi hili linajumuisha nchi zinazoongoza duniani katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi kidijitali. GTMI: Kipimo cha Ukomavu wa Serikali Kidijitali. Ripoti ya GTMI hutathmini ukomavu wa matumizi ya TEHAMA serikalini katika takriban nchi zote duniani, ikizingatia maeneo muhimu kama sera, sheria, miongozo, mifumo ya TEHAMA na utekelezaji wake. Toleo la 2025 la ripot...