TANZANIA YANG'ARA DUNIANI KUNDI LA VINARA WA SERIKALI KIDIGITALI - WORLD BANK 2025.
Na Hamida Ramadhani.
TANZANIA imeendelea kung’ara kimataifa baada ya Benki ya Dunia (World Bank – WB) kuitaja kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ukomavu wa juu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta ya umma.
Hatua hii ni uthibitisho wa mafanikio ya mageuzi ya kidijitali yanayoendelea kutekelezwa na Serikali katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya GovTech Maturity Index (GTMI) ya mwaka 2025, Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A – Ukomavu wa Juu wa Matumizi ya TEHAMA (Extensive GovTech Maturity).
Kundi hili linajumuisha nchi zinazoongoza duniani katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi kidijitali.
GTMI: Kipimo cha Ukomavu wa Serikali Kidijitali.
Ripoti ya GTMI hutathmini ukomavu wa matumizi ya TEHAMA serikalini katika takriban nchi zote duniani, ikizingatia maeneo muhimu kama sera, sheria, miongozo, mifumo ya TEHAMA na utekelezaji wake.
Toleo la 2025 la ripoti hii lilitolewa mwezi Desemba baada ya utafiti wa kina wa karibu mwaka mmoja.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kupata utambuzi huu, mwaka 2022, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri zaidi duniani, ikipanda kutoka nafasi ya 90 mwaka 2021 hadi nafasi ya 26 mwaka 2022, na kutoka Kundi B hadi Kundi A. Barani Afrika, Tanzania ilishika nafasi ya pili baada ya Mauritius na kuwa kinara wa Afrika Mashariki.
Nafasi ya Tanzania Barani Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti ya GTMI 2025, Tanzania ni moja kati ya nchi tano pekee barani Afrika zilizoingia kwenye kundi la juu la ukomavu wa TEHAMA serikalini.
Nchi nyingine ni Kenya, Misri, Uganda na Rwanda, jambo linaloionesha Tanzania kama kinara wa mageuzi ya kidijitali katika utawala wa umma.
Mafanikio haya yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kutumia teknolojia kuongeza ufanisi wa taasisi za umma, kuimarisha uwazi na kuongeza uwajibikaji kwa wananchi.
Mifumo ya Mikuu ya Serikali Yachochea Mafanikio.
Ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa mafanikio ya Tanzania yametokana kwa kiasi kikubwa na uwepo na matumizi madhubuti ya Mifumo ya Mikuu ya Serikali (Core Government Systems).
Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Mishahara (HCIMS), Ajira Portal, pamoja na mifumo ya kuunganisha na kubadilishana taarifa kati ya taasisi za umma.
Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus – GovESB) umetajwa kuwa mhimili muhimu unaowezesha taasisi za umma kubadilishana taarifa kwa usalama, ufanisi na kwa wakati, hatua iliyopunguza urudufu wa taarifa na kuharakisha utoaji wa huduma.
Ushirikishwaji wa Wananchi Kidijitali.
Katika eneo la Digital Citizen Engagement, Tanzania imetambuliwa kwa kuwekeza katika mifumo inayowawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika masuala ya utawala. Mfumo wa e-Mrejesho umetajwa kuwa chombo muhimu kinachowezesha wananchi kutoa maoni, malalamiko, ushauri na pongezi, na kupokea mrejesho kwa wakati.
Mfumo huu umeongeza uwazi, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali.

Mazingira Wezeshi ya GovTech.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa uwepo wa sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao (GovTech Enablers) umeweka mazingira rafiki ya utekelezaji wa miradi ya TEHAMA kwa mwelekeo mmoja wa kitaifa. Mazingira haya yameiwezesha Serikali kusimamia vyema rasilimali za TEHAMA na kuleta tija katika uwekezaji wa kidijitali.
Huduma za Serikali Mtandaoni.
Utoaji wa huduma za serikali kwa njia ya mtandao kupitia mifumo kama Mfumo Mkuu wa Malipo Serikalini (GePG), Mfumo wa Kitaifa wa Manunuzi ya Kielektroniki (NeST) na mifumo ya Serikali za Mitaa (TAUSI) umeongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi, uwazi na kwa gharama nafuu.
Mtazamo wa e-GA.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema kuwa matokeo hayo ni ushahidi wa mwelekeo sahihi wa taifa katika kujenga Serikali ya kidijitali.
Ameeleza kuwa Benki ya Dunia ilifanya utafiti huu kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa kutumia mbinu za Evidence-based GovTech Maturity Index Survey, huku akizitaka taasisi za umma kuendelea kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, kuunganisha mifumo yao na GovESB na kuimarisha matumizi ya mifumo ya ushirikishwaji wa wananchi.
Mafanikio haya yanaifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mageuzi ya kidijitali barani Afrika, na kuweka msingi imara wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za umma, kukuza uwazi, na kuimarisha uchumi wa kidijitali kwa maendeleo endelevu ya taifa.






Maoni