Na Lubango Mleka, Serengeti. MAWAKALA wa utalii 120 kutoka nchini Marekani wameonyesha kuvutiwa na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini Tanzania, hususani mandhari ya kuvutia, wanyamapori, na urithi wa utamaduni wa kipekee. Tukio hilo limejidhihirisha katika usiku wa Novemba 7, 2025 kwenye hafla ya chakula cha usiku iliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Mkoani Mara, iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuwakaribisha mawakala hao waliowasili nchini kwa ziara ya kutembelea vivutio vya utalii. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Excellent Guide Tours and Safaris, Justin Alfred, amesema; "Tumevutiwa sana na mandhari ya Tanzania, hasa wanyamapori kama tembo, twiga, simba na nyati. Nchi hii ni salama, wananchi wake ni wakarimu, watalii wasisite kuja kuitembelea." Amesema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha Tanzania inatambulika zaidi duniani kama kitovu cha utalii barani Afrika kutokana na urithi wake wa asili, utamaduni na vivutio vya ki...