BABA LEVO KUTUMIA MABANGO YA KAMPENI KUTENGENEZA MEZA ZA WAFANYABIASHARA KIGOMA MJINI
Na Hamida Ramadhan, Dodoma.
MBUNGE wa Kigoma Mjini Mheshimiwa Clayton Revocatus Chipando anayejulikana kwa jina la Baba Levo ameonyesha mfano wa ubunifu na uwajibikaji kwa kutumia mabango 80000 ya kampeni yaliyosalia baada ya uchaguzi kutengeneza meza zitakazotolewa bure kwa wafanyabiashara wadogo katika masoko ya Kigoma Mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari mbunge huyo Baba Levo amesema hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na kuonyesha kwamba hata vifaa vilivyotumika kisiasa vinaweza kuwa na faida kijamii endapo vitatumiwa kwa ubunifu.
Amesema badala ya mabango ya kampeni kubaki yakiharibu mazingira wameamua kuyageuza kuwa meza imara kwa ajili ya wafanyabiashara wa Kigoma ni njia ya kugeuza alama za siasa kuwa alama za maendeleo.
Meza hizo zitatolewa rasmi wiki ijayo katika mkutano mkubwa wa shukurani utakaofanyika Kigoma Mjini ambapo Baba Levo atawashukuru wananchi kwa imani waliyoonyesha kwake na kueleza mwelekeo wa uongozi wake mpya.
"Mpango wa kutumia mabango ya kampeni kwa manufaa ya wananchi ni ishara ya uongozi unaojali unaotumia kila rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya Kigoma Mjini, " Amesema baba Levo.
Aidha amesema Mkutano huo utahudhuriwa na wananchi viongozi mbalimbali na wasanii maarufu wageni wengine wakiwemo wasanii wa ndani Kigoma.
Pia amesema siku yakuapa atasindikizwa na mzee wake Diamond Platnumz Nasib Abdul ,mke wake mtoto wake Levo dada yake na Katibu wake.
Katika mkutano wake huo wa shukurani Baba Levo atazungumzia mipango ya maendeleo ya jimbo lake ikiwemo kuboresha barabara za mitaa ili kuondoa barabara za tope kuimarisha masoko ya jioni na kuongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake.
Aidha amethibitisha msimamo wake katika uchaguzi wa Spika wa Bunge akisema kura yake itaenda kwa Mheshimiwa Azan Zungu kutokana na uzoefu wake mkubwa huku akiunga mkono Mheshimiwa Daniel Silo kwa nafasi ya Naibu Spika.
Baba Levo pia ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa wananchi wote waliopata madhara wakati wa matukio ya hivi karibuni akisisitiza kuwa maandamano ni haki ya kikatiba lakini lazima yafanywe kwa amani.
" tunavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa ya kurejesha utulivu Lengo letu ni kujenga amani na maendeleo si migawanyiko," amesema.

Maoni