ZIMAMOTO YAWAKARIBISHA WANANCHI KUPATA ELIMU YA UOKOAJI KATIKA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA
Na Hamida Ramadhan, Dodoma.
WANANCHI wametakiwa kutumia fursa ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kutembelea banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata elimu ya kujikinga na majanga ya moto pamoja na mbinu za uokoaji wakati wa dharura.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yanayoendelea jijini Dodoma, Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalayaimisi, alisema banda la jeshi hilo limekuwa likitoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuokoa maisha na mali pindi majanga yanapotokea.
Amesema wananchi wanaofika katika banda hilo wanapata mafunzo kuhusu hatua za kuchukua kabla, wakati na baada ya kutokea kwa majanga ya moto pamoja na maafa mengine yanayohitaji huduma za uokoaji.
"Tunatumia maonesho haya kukutana moja kwa moja na wananchi na kuwapa elimu itakayowasaidia kujikinga na majanga pamoja na kuelewa namna ya kushirikiana na jeshi la zimamoto wakati wa dharura," amesema.
Nzalayaimisi ameleza kuwa elimu hiyo ni sehemu ya mkakati wa jeshi hilo wa kupunguza athari za majanga kwa kuwajengea wananchi uelewa wa tahadhari na hatua sahihi za kuchukua wanapokabiliwa na matukio mbalimbali ya hatari.
Aidha, amesema maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanatoa nafasi kwa taasisi za umma kueleza huduma wanazotoa na kusikiliza maoni ya wananchi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma.
Ameongeza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Nzalayaimisi amewahimiza wananchi kutoka mikoa mbalimbali kutembelea banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata elimu ya kinga dhidi ya moto, uokoaji wa mali wakati wa mafuriko na namna ya kukabiliana na majanga mengine yanayoweza kutokea katika mazingira yao.
Amesema elimu inayotolewa na jeshi hilo ni muhimu kwa kila mwananchi kwa kuwa usalama wa maisha na mali huanza na uelewa wa hatua za tahadhari kabla ya janga kutokea.

Maoni