WAKAZI USUNGA WAMPONGEZA RAIS SAMIA













Na Allan Kitwe, Tabora. 

WAKAZI wa Kijiji Cha Usunga, Kata ya Usunga Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi wa maji safi na salama ya kunywa.

Wametoa pongezi hizo jana kwenye shamra shamra za kilele cha Maadhimisho ya Miaka 58 tangu kuanzishwa kwa Kijiji hicho ambacho kimekuwa mfano wa kuigwa kwa kudumisha mila, utamaduni, mshikamano na ulinzi wa jadi.

Akizungumza na wananchi kwenye shamrashamra hizo zilizopambwa na ngoma, burudani, chakula cha asili na vinywaji, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho James Mgulu ameishukuru serikali kwa kumaliza kero ya maji katika Kata hiyo.

Amefafanua kuwa tangu kuanzishwa kwake wakazi wa Kijiji hicho wameendeelea kunufaika na mambo mengi mazuri yanayofanywa na serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo kudumisha umoja, amani na mshikamano.  

Akielezea kiini cha sherehe hiyo, Diwani wa Kata hiyo Jackson Mbasha amesema kuwa utaratibu huo ulianzishwa na wazee waasisi, lengo likiwa kudumisha mila, tamaduni, umoja na mshikamano wao, ulinzi shirikishi na kuenzi mazuri yanayofanywa na serikali.

Amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia na watangulizi wake kwa kuhakikisha Kata hiyo yenye vijiji 4 vya Usunga, Urafiki, Isanjandugu na Mwanamkata na vitongoji 16 inapata huduma bora ikiwemo maji safi na umeme.

‘Tunaishukuru sana serikali kwa kuboresha huduma za kijamii katika Kata yetu, wananchi sasa wanapata huduma bora za afya, maji, umeme na miundombinu ya elimu katika shule zote imeendelea kuboreshwa, tunamshukuru sana,’ ameeleza.

Akifunga sherehe hizo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sikonge Anna Chambala amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia kwa kupeleka mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo katika Kata hiyo.

Amewataka kulinda miundombinu ya miradi yote inayotekelezwa na serikali ili iwanufaishe wao na vizazi vyao na kuendelea kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano wao ili kuenzi maono mazuri ya wazee wao na kudumisha ulinzi wa jadi








Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.