WAKAZI USUNGA WAFURAHIA MRADI WA MAJI

 



Na Allan Kitwe, Sikonge. 

WAKAZI wa Kijiji Cha Usunga, Kata ya Usunga Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi wa maji safi na salama ya kunywa.

Wametoa shukrani hizo kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 58 tangu kuanzishwa kwa Kijiji hicho zilizofanyika jana kwenye uwanja wa CCM (Centre) na kueleza bayana kuwa serikali imemaliza kilio chao cha muda mrefu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho James Mgulu ameeleza kuwa mradi wa maji katika Kijiji hicho umeleta neema, furaha na shangwe kwa wananchi kwa sababu familia zao zilikuwa zinapata shida sana kwa kukosa maji safi na salama.

‘Tuna kila sababu ya kuishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu wa maji na miradi mingine ya maendeleo, wananchi sasa wana amani tele, na maisha yao yamekuwa bora zaidi’, ameeleza.

 Ameongeza kuwa wanapoadhimisha sherehe hiyo kila mwaka wanalenga kudumisha mila, utamaduni, upendo, mshikamano na ulinzi wa kaya zao, na mwaka huu wanasherehekea wakiwa na furaha ya maendeleo waliyopata.

Diwani wa Kata hiyo Jackson Mbasha ameeleza kuwa serikali imewafanyia wakazi wa Kata hiyo mambo mengi na mazuri hivyo wana kila sababu ya kumshukuru sana Rais Samia kwa dhamira yake ya kumaliza kero za wananchi.

‘Nampongeza sana Rais Samia na wasaidizi wake kwa kuhakikisha Kata hii yenye vijiji 4 vya Usunga, Urafiki, Isanjandugu na Mwanamkata na vitongoji 16 inapata huduma zote za kijamii, maji, umeme, afya na barabara’, ameeleza.

Serikali imetuboreshea huduma za kijamii kwa kiasi kikubwa sana, wananchi sasa wanapata huduma bora za afya, maji, umeme na miundombinu ya elimu katika shule zote imeendelea kuboreshwa, changamoto kidogo ipo kwenye barabara tu.

Akifunga sherehe hizo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sikonge Anna Chambala amepongeza ushirikiano mzuri wa Viongozi wa Serikali ya Kijiji, Kata na Chama na kushauri Kata zingine kuiga mfano huo.

Aidha amepongeza Kata hiyo kwa kufanya sherehe hiyo kila mwaka kwani inasaidia kudumisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwao, hivyo akawataka kuendeleza maono hayo ya wazee wao.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.