UNYONYAJI WA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI BADO WATAJWA KUWA CHANGAMOTO
Na Jasmine Shamwepu, Habari Kamili Blog-Dodoma.
MATUKIO ya unyonyaji, mishahara duni na ukosefu wa mikataba ya ajira yameendelea kutajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri ustawi wa wafanyakazi wa majumbani nchini, hali inayochochea wito wa kuwepo kwa hatua zaidi za kuwalinda.
Hayo yameelezwa na wadau wa sekta ya ajira wakati wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kazi za Majumbani wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30 uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani nchini, Zanini Athumani, amesema pamoja na umuhimu wa kazi za majumbani katika jamii, bado baadhi ya wafanyakazi wanakabiliwa na mazingira yasiyozingatia haki zao za msingi.
Amesema changamoto hizo zinajumuisha kucheleweshwa kwa mishahara, kutokuwepo kwa mikataba ya kazi na kukosekana kwa mifumo madhubuti ya kushughulikia malalamiko wanayokumbana nayo.
“Wafanyakazi wengi wa majumbani bado wanahitaji ulinzi zaidi ili waweze kufanya kazi zao kwa usalama na kupata stahiki zao kwa wakati,” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la CVM, Laura Vallesi, amesema wanawake na wasichana ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa changamoto zinazohusiana na kazi za majumbani, hususan katika maeneo ambayo hayana mifumo imara ya ulinzi wa wafanyakazi.
Alisema bado kuna haja ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu haki za wafanyakazi wa majumbani pamoja na madhara ya ajira za watoto na usafirishaji haramu wa binadamu.
Naye Meneja Miradi wa Shirika la Wote Sawa, Jackline Mujunangoma, alisema baadhi ya waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu huishia kufanya kazi za ndani katika mazingira magumu yanayowanyima haki za msingi ikiwemo elimu na usalama.
Amesema mashirika ya kiraia yanaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha waathirika hao kurejea kwenye maisha ya kawaida kupitia elimu, mafunzo ya ufundi na huduma za ushauri.
Katibu Mkuu wa CHODAWU, Said Wamba, amesema kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa wafanyakazi wa majumbani ili kuhakikisha wanapata haki sawa na wafanyakazi wa sekta nyingine.
Amesema ushirikiano wa wadau mbalimbali umeanza kuzaa matunda katika kuboresha hali ya wafanyakazi hao, lakini bado juhudi zaidi zinahitajika ili kukabiliana na changamoto zilizopo.
Wadau hao wameeleza kuwa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kazi za Majumbani utakuwa chachu ya kuimarisha mazingira ya kazi, kuongeza usalama wa wafanyakazi na kupunguza vitendo vya unyonyaji vinavyoripotiwa katika sekta hiyo.




Maoni