TANZANIA IPO TAYARI KUPOKEA AFCON 2027

 


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma. 

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo, amesema maandalizi ya kuelekea Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yanaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kupokea na kuandaa mashindano hayo kwa mafanikio.

Sillo ametoa kauli hiyo wakati wa Bonanza la Bunge (Bunge Grand Bonanza) lililofanyika jijini Dodoma, ambapo amesema kaulimbiu ya bonanza hilo inayohusiana na AFCON 2027 ni ishara ya namna Watanzania wanavyoendelea kuhamasika na kujiandaa kwa tukio hilo kubwa la kimichezo.

Amesema maandalizi yanayoendelea kufanywa na Serikali, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya michezo na huduma nyingine muhimu, yanaonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo ya kihistoria.

“AFCON 2027 ni fursa kubwa kwa Tanzania kujitangaza kimataifa kupitia sekta ya michezo. Sisi kama Bunge tutaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha maandalizi yanaenda kama yalivyopangwa na mashindano yanafanyika kwa mafanikio,” amesema Sillo.

Ameongeza kuwa bonanza hilo limekuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, kushiriki michezo na kuimarisha afya zao, sambamba na kukuza mshikamano wa kijamii.

Kwa upande mwingine, ametoa pongezi kwa CRDB Bank kwa mchango wake katika kudhamini bonanza hilo kwa miaka kadhaa, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa ushiriki wa wadau mbalimbali na mafanikio ya tukio hilo.

Sillo amesema ushirikiano kati ya taasisi za umma, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kukuza michezo nchini na kuleta manufaa mapana ya kijamii na kiuchumi kwa Taifa.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.