SANGA AIPONGEZA CRDB KWA KUDHAMINI BUNGE BONANZA MIAKA MITANO MFULULIZO



Na Jasmine Shamwepu, Dodoma. 

MWENYEKITI wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, ameipongeza CRDB Bank kwa kuendelea kuwa mdhamini mkuu wa Bunge Bonanza kwa miaka mitano mfululizo, akisema mchango wa benki hiyo umekuwa nguzo muhimu katika mafanikio na ukuaji wa tukio hilo kila mwaka.

Akizungumza katika Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Sanga amesema ushirikiano wa CRDB umechangia kuifanya shughuli hiyo kuwa zaidi ya tukio la michezo, kwa kuwa imekuwa jukwaa la kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano mema miongoni mwa wabunge, watumishi wa Bunge na wadau mbalimbali.

Amesema udhamini wa benki hiyo umewezesha bonanza hilo kuendelea kukua na kuvutia ushiriki mkubwa zaidi mwaka hadi mwaka, hali inayodhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi katika maendeleo ya jamii.

“Kwa mwaka wa tano mfululizo CRDB imeendelea kusimama nasi katika kufanikisha Bunge Bonanza. "

 Tunatoa shukrani za dhati kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Abdulmajid Nsekela, pamoja na menejimenti yote kwa kuendelea kuunga mkono jitihada hizi zinazolenga kuimarisha umoja, afya na ustawi wa jamii,” amesema Sanga.

Ameongeza kuwa CRDB imeendelea kuonyesha mfano wa taasisi inayojali maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji wake katika michezo na shughuli mbalimbali za kijamii zinazowagusa Watanzania.

Sanga pia ametambua mchango wa viongozi mbalimbali wa benki hiyo, akiwemo Tully Mwambapa, kwa kuendelea kusukuma mbele ajenda ya maendeleo kupitia michezo na programu nyingine zinazochochea ustawi wa jamii.

Aidha, amesema hatua za CRDB za kuendeleza diplomasia ya uchumi ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo kupanua shughuli zake katika masoko ya kikanda kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zinaonesha dhamira ya benki hiyo katika kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Afrika Mashariki na Kati.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa aina hiyo una mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya Taifa na kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.