MIUNDOMBINU CHUO CHA NYUKI TABORA YABORESHWA
Na Allan Kitwe, Tabora.
CHUO Cha Ufugaji Nyuki (BTI) Tabora kimeendelea kuboresha miundombinu yake kwa kujenga jengo jipya la kisasa la mihadhara linalogharimu zaidi ya shilingi milioni 500, utekelezaji mradi huu umefikia zaidi ya asilimia 48.
Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Chuo hicho Semu Daud alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake, ambapo ameeleza kuwa jengo hilo litaboresha ufundishaji wa wakufunzi na kutatua changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa chuoni hapo.
Amefafanua kuwa ujenzi wa jengo hilo unafadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania (TAFF) ambao wametoa kiasi cha shilingi milioni 500 sawa na asilimia 82 huku shilingi milioni 92 sawa na asilimia 20 zikitoka kwenye mfuko wa chuo.
Ukumbi huo utakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa wakati mmoja hivyo kukamilika kwake kutatoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kujiunga na fani ya ufugaji nyuki.
Mkuu amedokeza kuwa kupitia mradi huo mbali na wanafunzi kuongezeka chuoni hapo pia utasaidia kufanikisha utekelezaji shughuli nyingine za kimaendeleo ikiwemo mikutano na mihadhara ya kitaaluma.
Semu ameongeza kuwa chuo kimeendelea kukamilisha ufungaji mashine za kisasa kwenye karakana ya mbao inayotumika kutoa mafunzo kwa vitendo ili kuwaongezea ufanisi wahitimu na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Amefafanua kuwa chuo hicho ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kilichoanza kama Kituo cha Utafiti wa masuala ya ufugaji nyuki mwaka 1949 na mwaka 1978 serikali ilikibadili na kuwa Chuo cha Mafunzo ya Nyuki.
Awali serikali ilihamisha shughuli za Chuo hicho kutoka Tabora kwenda Tengeru, Olmotonyi Mkoani Arusha ila mwaka 2020 serikali ikarejesha tena shughuli za Chuo hicho Mkoani Tabora ambapo chuo kinaendelea hadi sasa.
Chuo hicho kinatoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada, mafunzo ya muda mfupi yanaanzia wiki 1 hadi 3 ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalaamu, utafiti wa ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira.




Maoni