EWURA CCC YATOA MWANGA KWA WANANCHI WASIOJUA PAKUPELEKA MALALAMIKO

 


Na Hamida Ramadhan, Dodoma. 

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA CCC) limesema zaidi ya wananchi 500 wametembelea banda lake katika Wiki ya Utumishi wa Umma na kupata elimu, ushauri pamoja na fursa ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu huduma za maji, umeme na gesi.

Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa EWURA CCC, Amani Mbogo, amesema baraza hilo lina jukumu la kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za nishati na maji kwa kuhakikisha sauti zao zinasikika na changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi.

Akizungumza katika Wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea jijini Dodoma, Mbogo amesema wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na huduma za maji na nishati, lakini hawafahamu mahali pa kupeleka malalamiko yao ili kupata msaada.

“Tumepokea wananchi wengi waliokuja kupata elimu kuhusu majukumu ya EWURA CCC, kutoa maoni, ushauri na kuwasilisha malalamiko yao. Mwitikio umekuwa mkubwa na unaonyesha umuhimu wa kuendelea kuwafikia watumiaji wa huduma hizi,” amesema Mbogo.

Amesema malalamiko mengi yaliyowasilishwa yanahusu upatikanaji wa huduma za maji na umeme, ambapo baadhi ya wananchi wameunganishwa moja kwa moja na taasisi husika ikiwemo TANESCO ili kupata ufumbuzi wa changamoto zao.

Mbogo amesema baada ya kumalizika kwa Wiki ya Utumishi wa Umma, EWURA CCC itaendelea kufuatilia malalamiko yaliyowasilishwa ili kuhakikisha wahusika wanapata majibu na huduma stahiki.

Kwa upande wa matumizi ya gesi, amesema wananchi waliotembelea banda hilo wanapaswa kupima mitungi ya gesi kwa kutumia mzani ili kuhakikisha kama ujazo upo sahihi wa mitungi. 

“Mafanikio makubwa ambayo tumeyaona ni kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu EWURA CCC na huduma tunazotoa. Wengi hawakuwa wanafahamu kuwa wana sehemu maalumu ya kuwasilisha malalamiko yao na kupata msaada,” amesema.

Naye mkazi wa eneo la Chimuli, Kata ya Makole jijini Dodoma, Tostar Ceprian, amesema amewasilisha kero ya maji taka ambayo imekuwa ikiwasumbua wakazi wa eneo hilo kwa zaidi ya miaka mitatu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema wakati wa msimu wa mvua maji hayo hujaa na kuingia ndani ya nyumba za wananchi, hali inayosababisha usumbufu mkubwa na kuhatarisha afya za wakazi wa eneo hilo.

“Hii ni changamoto ya muda mrefu. Tumekuwa tukilalamika mara kwa mara lakini hatukupata majibu ya kuridhisha. Baada ya kufika hapa nimesikilizwa na malalamiko yetu yamepokelewa kwa ajili ya kufuatiliwa,” amesema Ceprian.

Ameeleza matumaini yake kuwa hatua iliyochukuliwa na EWURA CCC itasaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo na kuondoa adha inayowakabili wananchi wa Makole kwa muda mrefu.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.