ASMA MWINYI FOUNDATION YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU
Na Jasmine Shamwepu, Dodoma.
MWANZILISHI na Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation, ambaye pia ni Mbunge wa Welezo, Unguja, Asma Ally Hassan Mwinyi, ameungana na watoto wenye usonji (Autism), ugonjwa wa Down Syndrome na mtindio wa ubongo (Cerebral Palsy), pamoja na wazazi wao, kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuwapa fursa ya kusikika na kujadili changamoto zinazowakabili.
Katika maadhimisho hayo ya Juni 16, Asma Mwinyi Foundation kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe iliandaa ziara maalumu ya watoto hao na wazazi wao katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, ambapo walipata nafasi ya kuzungumza na viongozi na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha ya kila siku.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Asma alisema lengo la kuwakutanisha watoto hao na wazazi wao ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kuondoa unyanyapaa na kuhamasisha upatikanaji wa huduma bora za afya na matibabu kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Alisema watoto wenye usonji, Down Syndrome na mtindio wa ubongo bado wanakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kutengwa, kukosa uelewa kutoka kwa jamii na gharama kubwa za matibabu.
“Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni fursa ya kuwakumbusha Watanzania kuwa watoto hawa wana haki sawa na watoto wengine. Wanahitaji kupendwa, kulindwa, kuelimishwa na kupewa nafasi ya kufikia ndoto zao,” alisema Asma.
Mbali na kupata nafasi ya kuzungumza na viongozi, watoto hao na wazazi wao pia walipata chakula cha mchana kama sehemu ya kuenzi na kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika.
Wakati huo huo, wawakilishi kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe walipongeza ushirikiano uliopo kati ya hospitali hiyo na Asma Mwinyi Foundation katika kusaidia watoto wenye usonji, Down Syndrome na mtindio wa ubongo.
Walisema ushirikiano huo umechangia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mahitaji ya watoto hao na kuwasaidia kupata huduma muhimu za afya na matibabu.
Baadhi ya wazazi walioshiriki katika maadhimisho hayo walieleza changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo unyanyapaa, gharama kubwa za matibabu na ukosefu wa huduma maalumu katika baadhi ya maeneo.
Wametoa wito kwa jamii kuacha mitazamo hasi dhidi ya watoto wenye mahitaji maalumu na badala yake kushiriki katika kuwajumuisha katika shughuli za kijamii na maendeleo.
Maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa jukwaa la kuibua sauti za watoto wenye mahitaji maalumu na familia zao, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa kujenga jamii jumuishi inayolinda haki za kila mtoto bila kujali hali yake ya kiafya au maendeleo
.








Maoni