SIKU YA NYUKI DUNIANI’ YAADHIMISHWA KITAIFA TABORA

 






Na Allan Kitwe, Tabora. 

MAADHIMISHO ya Siku ya Nyuki Duniani yanayoyohusisha utundikaji mizinga, maonesho ya bidhaa na mazao ya nyuki yameanza leo katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Vita Mjini Tabora na kuvuta umati mkubwa wa wananchi.

Wakizungumza kwenye maadhimisho hayo wakazi wa Tabora wameeleza kufurahishwa na tukio hilo kwa kuwa linawapa fursa wageni kutembelea Mkoa huo na kuonja utamu wa asali inayozalishwa katika misitu ya Mkoa huo.

Daud Elisha, mjasiriamali mkazi wa Kata ya Kanyenye, Halmashauri ya manispaa ya Tabora ameeleza kuwa zao la asali ni miongoni mwa mazao ya kujivunia yanayozalishwa katika Mkoa huo na kuuzwa kwa bei kubwa ndani na nje ya nchi.

‘Haya maadhimisho ni fursa muhimu sana kwa wana Tabora kuuza asali yao na kupanua wigo wa uzalishaji zao hilo katika Wilaya zote za Mkoa huu, hivyo kuwaneemesha zaidi kiuchumi’, amesema.

Amina Madereka, mjasiriamali anayejishughulisha na utundikaji mizinga na uuzaji asali katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ameeleza kuwa kupitia maadhimisho haya soko la asali na mazao ya nyuki kutoka Tabora litapaa zaidi.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. John Mboya ameeleza kuwa maadhimisho hayo yamelenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi, wadau na taasisi mbalimbali kwenye shughuli za ufugaji nyuki ili kujiongezea kipato na kuchangia pato la taifa.

Amedokeza kuwa maadhimisho hayo yanayofanyika kuanzia Mei 19 hadi 22 mwaka huu yatashirikisha viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali, wadau wa maendeleo, wafugaji nyuki, wanafunzi pamoja na wananchi kwa ujumla.

Ameongeza kuwa nyuki wana mchango mkubwa katika uhifadhi wa bio anuai, uchavushaji wa mazao ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato kupitia bidhaa zitokanazo na nyuki ikiwemo asali, nta na gundi. 

‘Mkoa wa Tabora unaongoza kwa uzalishaji wa asali yenye ubora nchini, ukichangia takriban asilimia 50 ya asali yote inayozalishwa Tanzania, pamoja na mazao mengine yatokanayo na nyuki’, ameeleza.

Dkt Mboya ameongeza kuwa ubora wa asali ya Tabora unatokana na uwepo wa misitu ya miti ya jamii ya Miyombo, ambayo imeelezwa kuwa chanzo kikuu cha asali ya asili na yenye viwango vya juu vya ubora.

Dkt Mboya amesisitiza kuwa serikali inahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika ufugaji nyuki wa kisasa ili kuongeza ajira, kipato na kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu sambamba na kulinda misitu na mazingira.

Maadhimisho hayo yatapambwa na utundikaji mizinga, matembezi ya kutangaza Asali ya Tabora (Asali Walkerthon), midahalo, maonesho ya bidhaa na teknolojia ya nyuki na elimu ya umuhimu wa nyuki na uhifadhi wa mazingira.

“Kaulimbiu ya maadhimisho haya ya mwaka huu ni ‘Uhifadhi wa Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Taifa Letu’.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.