RC TABORA APEWA TUZO MAALUMU




Na Allan Kitwe, Tabora

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora kimetoa tuzo maalumu kwa Mkuu wa Mkoa huo Paul Matiko Chacha kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wake katika suala zima la kusimamia maendeleo ya Mkoa huo.

Tuzo hiyo imetolewa juzi kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya  Mkoa baada ya Wajumbe wa mkutano huo kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Kiongozi huyo hivyo kupendekeza apewa tuzo katika kikao hicho.

Awali, akielezea tuzo hiyo, Katibu wa CCM Mkoa Wilson Nkambaku amesema kuwa pendekezo la kutoa tuzo hiyo lilitolewa na Wajumbe katika Kikao kilichopita, hivyo chama kimelifanyia kazi na sasa wapo tayari kumkabidhi.

Ameongeza kuwa chama pia kitatoa tuzo kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mheshimiwa Said Juma Nkumba kama ishara ya kutambua kazi yake njema ya kuimarisha, kudumisha na kujenga mshikamano thabiti ndani ya chama.

Akikabidhi tuzo kwa Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Said Juma Nkumba amesema kuwa Chama kimeridhishwa na kazi yake, anatekeleza wajibu wake kwa vitendo, amebeba dhamana ya chama na serikali, hatuna mashaka naye.  

‘Hiki ni Kikao Maalumu cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ambacho mbali na mambo mengine kimeona umuhimu wa kutoa tuzo hii kwa Mkuu wetu wa Mkoa, tunajivunia uwepo wake katika Mkoa huu, anajali maslahi ya chama’, amesema.

Nkumba ameongeza kuwa RC na timu yake ya Watumishi wamekuwa chachu ya mafanikio makubwa tunayoyashuhudia katika Mkoa huu na Wilaya zake zote, wamekuwa mstari wa mbele kwenye utekelezaji wa ilani ya chama.

RC Chacha amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu na chama kwa ujumla kwa kuwaongoza vema katika utendaji wao na kuwapa ushirikiano ambao umeendelea kuleta tija kubwa kwa maendeleo ya wananchi.

‘Mimi na Ma-DC wote tunaheshimu dhamana tuliyopewa na serikali hii ya CCM, tutaendelea kujituma zaidi katika utumishi wetu ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na kujitoa kwa chama pia’, ameeleza.   

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) wa Mkoa huo Mohamed Nassoro Hamdan amesema kuwa kazi nzuri inayofanywa na Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa imeendelea kukiheshimisha Chama katika Mkoa huo.

Amewataka wanaCCM na Viongozi wote waliopewa dhamana  kuendelea kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha yale yote yanayotekelezwa na serikali yanawanufaisha wananchi.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.