MANISPAA TABORA YATOA MOTISHA KWA WALIMU

 


Na Allan Kitwe, Tabora. 

HALMASHAURI ya manispaa Tabora imetoa motisha kwa walimu na shule za sekondari zilizofanya vizuri zaidi katika masomo mbalimbali kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha 4, 6na ule wa kujipima wa kidato cha 2 kwa mwaka 2025.

Akitoa taarifa kwenye kikao cha baraza la madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt John Pima, ameeleza kuwa wametoa motisha hiyo ili kuwatia moyo walimu na shule zao ili waendelee kufanya vizuri zaidi.

Amefafanua kuwa kwa mwaka wa masomo 2025 halmashauri ya manispaa hiyo ilishika nafasi ya kwanza Kimkoa kati ya halmashauri 8 katika mitihani ya taifa ya kidato cha 6, 4 na upimaji wa kidato cha 2.

Pima ameongeza kuwa kwa ujumla shule zote katika manispaa hiyo zilifanya vizuri katika mitihani hiyo ikilinganishwa na mwaka uliopita sababu kuu ikitajwa kuwa ni juhudi na weledi wa walimu katika kufundisha watoto hao.

Amedokeza kuwa katika mitihani ya kidato cha 4 walimu wa shule za sekondari za kata ambao masomo yao yalipata ufaulu mkubwa zaidi wamezawadiwa cheti na fedha taslimu sh 100,000.

Walimu hao ni Agnes Ndele wa shule ya sekondari Nkumba (Kiswahili), David Mwalwisi wa shule ya sekondari Nyamwezi (Hisabati), Veronika Maziku shule ya sekondari Fundikira (Biolojia) na Msafiri Mkinde wa Nyamwezi sekondari (Kemia).

Wengine ni Boaz Ewiso (Uraia), Ruben Lishinu (Jiografia), Boniphace Wambura (Fizikia) wote kutoka Nkumba sekondari, Paulo Kamlali wa Nyamwezi sekondari (Historia) na Damian Ndibalema wa Misha sekondari (Kiingereza).

Ametaja shule zenye idadi kubwa ya watoto zilizofanya vizuri katika mitihani hiyo na kuzawadiwa cheti na sh laki 3 kuwa ni Milambo sekondari, Ipuli sekondari na Kazima sekondari.

Shule 3 zilizoshika nafasi ya 1-3 kwa matokeo ya jumla na kuzawadiwa cheti na fedha taslimu kuwa ni Tabora Wavulana, Tabora Wasichana na Itaga sekondari.

Shule nyingine zilizofanya vizuri na kuzawadiwa cheti na fedha taslimu ni Nkumba sekondari, Itonjanda sekondari na na Nyamwezi sekondari.

Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo GhulamDewji Remtullah amepongeza Ofisi ya Mkurugenzi kwa kuzawadia shule na walimu waliofanya vizuri katika masomo yao na kubainisha kuwa zawadi hizo zitaongeza ushindani katika shule zote.

Amesisitiza kuwa wataendelea na utaratibu huo ili kuinua zaidi kiwango cha ufaulu kwa shule zote za sekondari na msingi katika manispaa hiyo.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.