WITO WATOLEWA KUIMARISHA UDHIBITI WA MAGONJWA YA MAZINGIRA
Na Mwandishi Wetu, Morogoro.
SERIKALI imetoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali ili kudhibiti magonjwa yanayotokana na mazingira, hatua inayolenga kulinda afya ya jamii na kuzuia milipuko ya magonjwa.
Rai hiyo imetolewa Aprili 18, 2026, mkoani Morogoro katika kikao cha kuandaa mwongozo wa ufuatiliaji wa viashiria vya mazingira na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Otilia Gowelle,
Dkt. Gowelle amesema sekta zinazopaswa kushirikiana kuwa ni pamoja na afya ya mazingira, maji, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Ubunifu, maelewano na ushirikiano ni nguzo muhimu katika kuilinda nchi dhidi ya magonjwa yatokanayo na mazingira hivyo wajibu wetu kuhakikisha mwongozo huu unatumika kuleta mabadiliko chanya ya afya ya jamii” amesema Dkt. Gowelle.
Gowelle, amepongeza timu ya wataalamu kwa juhudi za kukusanya na kuandaa maarifa yao katika mwongozo unaozingatia sera zilizopo, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa viashiria vya mazingira.
Aliongeza kuwa, hatua hiyo inaonyesha uwezo wa wataalamu wa ndani wa kutatua changamoto kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Kikao hicho kimetajwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji wa viashiria vya mazingira, ambao utasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kupanga mikakati madhubuti ya kinga na kuboresha huduma za afya kwa jamii.







Maoni