WATAALAMU WA AFYA, SANYANSI ONGEZENI JUHUDI MATUMIZI YA TEKNOLOJIA

 



Na Jasmine Shamwepu, Dodoma. 

SELIKALI  imewataka wataalamu wa afya na sayansi nchini kuongeza juhudi katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba, ili kuboresha huduma za afya na kusaidia utoaji wa haki jinai kwa ufanisi zaidi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati akifungua mkutano wa kisayansi wa teknolojia ya vinasaba uliofanyika jijini Dodoma, uliowakutanisha wataalamu wapatao 400 kutoka sekta mbalimbali.

Amesema teknolojia ya vinasaba imekuwa mhimili muhimu katika huduma za kisasa za afya, ikisaidia katika upandikizaji wa viungo kama figo na uroto wa mifupa, pamoja na kuboresha utambuzi wa magonjwa na utoaji wa tiba za kisasa zikiwemo tiba jeni na chanjo.

Mbali na sekta ya afya, amesema teknolojia hiyo imeleta mapinduzi katika mfumo wa haki jinai kwa kuwezesha upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi unaosaidia uchunguzi na utoaji wa haki kwa usahihi zaidi.

Dkt. Samizi ameeleza kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika kuimarisha sekta hiyo kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, vifaa na rasilimali watu.

Amebainisha kuwa ujenzi wa maabara ya kisasa ya vinasaba vya binadamu unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 16.73, sambamba na ununuzi wa mitambo mitano ya uchunguzi wa vinasaba yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ikiwemo matumizi madogo ya teknolojia hiyo katika uchunguzi wa magonjwa ya kurithi na adimu, pamoja na uelewa mdogo wa matumizi ya tiba binafsishi na tiba jeni.

Aidha, amewataka wataalamu kuzingatia Sheria ya Udhibiti wa Vinasaba vya Binadamu, akionya dhidi ya usafirishaji holela wa sampuli za vinasaba nje ya nchi bila kufuata taratibu, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa taarifa za Watanzania.

Kwa ujumla, amesisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana na kuibua mapendekezo yatakayosaidia serikali kuimarisha zaidi matumizi ya teknolojia ya vinasaba kwa manufaa ya taifa.










Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.