SERIKALI YAWEKA MKAZO SEKTA YA MADINI KUPITIA VIPAUMBELE NANE 2026/2027

 


Na Hamida Ramadhan,

DODOMA

WIZARA ya Madini imeweka bayana mkakati wa vipaumbele nane kwa mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuifanya sekta hiyo kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha rasilimali zinasimamiwa kwa ufanisi zaidi.

Akiwasilisha mpango wa bajeti bungeni, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema serikali imejipanga kuimarisha utafiti wa madini ili kubaini maeneo mapya yenye utajiri na kuongeza upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazovutia wawekezaji zaidi.

Alieleza kuwa mkazo pia utawekwa kwenye uongezaji thamani wa madini kwa kuyachakata ndani ya nchi, jambo litakaloongeza mapato ya taifa, kufungua ajira mpya na kuinua thamani ya mauzo ya nje.

Katika kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi, wizara inalenga kuongeza ushiriki wao katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, hususan kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo na wa kati kupitia mafunzo na uwezeshaji wa kitaalamu.

Aidha, serikali itaendelea kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo rasmi ya uchimbaji, mitaji pamoja na teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kupunguza shughuli zisizo rasmi.

Kwa upande wa mapato, Waziri Mavunde alisisitiza kuwa juhudi zitaongezwa kudhibiti utoroshaji wa madini na kuhakikisha kodi na tozo zote zinalipwa ipasavyo, hatua itakayoongeza mapato ya serikali.

Sambamba na hilo, masoko ya madini yataimarishwa ili kuweka mazingira ya biashara yenye uwazi na ushindani wa haki, huku jitihada zaidi zikifanywa kuvutia uwekezaji kwa kuboresha sera na kurahisisha taratibu za utoaji wa leseni.

Katika kulinda mazingira na maisha ya wachimbaji, wizara pia imepanga kuimarisha usimamizi wa usalama migodini na kuhakikisha sheria na kanuni za mazingira zinafuatwa kikamilifu.

Mpango huo unaonesha dhamira ya serikali ya kuiimarisha sekta ya madini ili iwe mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi wa taifa.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.