SERIKALI YAKIRI UHABA WA WATAALAMU, MALIPO YALALAMIKIWA

 



Na Jasmine Shamwepu, Dodoma. 

NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema serikali inatambua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa usingizi na ganzi nchini, akibainisha kuwa kwa sasa kuna takribani wataalamu 2,950 wanaohudumia hospitali zaidi ya 800.

Amesema serikali imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na upungufu huo kwa kuongeza nafasi za mafunzo, hususan katika ngazi ya stashahada, ili kuongeza idadi ya wataalamu na kuboresha utoaji wa huduma za afya.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha tunakuwa na wataalamu wa kutosha watakaoweza kutoa huduma salama na kupunguza vifo vinavyotokana na upasuaji, hasa kwa mama na mtoto,” amesema.

Hata hivyo, wataalamu wa huduma ya usingizi na ganzi wameiomba serikali kuhakikisha wanalipwa kwa wakati malipo ya saa za ziada wanazofanya, wakisema kucheleweshewa stahiki hizo kunapunguza ari ya kazi na kuhatarisha ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Akizungumza katika kongamano la nne la Chama cha Wataalamu wa Dawa za Usingizi, Ganzi na Upasuaji Tanzania (TANPA), rais

 wa chama hicho, Dkt. Julia Mahamba, amesema uhaba wa wataalamu hao unawalazimu kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi ya kawaida, hasa katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto wakati wa upasuaji.

“Tunafanya kazi kwa muda mrefu ili kuhakikisha huduma zinaendelea, lakini hatupati malipo ya saa za ziada kwa wakati, hali inayopunguza morali ya kazi na inaweza kuathiri ubora wa huduma,” amesema.

Kwa upande wake, Dkt. Evans Pesa, amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kujadili mikakati ya kuboresha huduma salama za usingizi na ganzi nchini ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora zaidi.

Kwa ujumla, wataalamu hao wameisisitiza serikali kuzingatia ustawi wao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wakiamini kuwa hatua hiyo itaimarisha sekta ya afya nchini.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.