SERIKALI YAJA NA MKAKATI MPYA WA KULINDA FEDHA ZA USHIRIKA

 


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma. 

SERIKALI imezindua mkakati mpya wa kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika nchini, ukiwa na lengo la kulinda fedha za wanachama na kuongeza uwajibikaji kwa viongozi.

Akizungumza jijini Dodoma katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Ushirika, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema kuwa sekta ya ushirika ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, ikizingatiwa kuwa inazungusha fedha zinazokadiriwa kufikia trilioni sita.

Amesema kuwa ili kuhakikisha fedha hizo zinalindwa ipasavyo, serikali inapanga kuimarisha mifumo ya ukaguzi, usimamizi na uwazi, sambamba na kuanzisha miundombinu maalum ya kushughulikia makosa yanayohusiana na vyama vya ushirika.

“Lengo letu ni kuona vyama vya ushirika vinakuwa salama, vinawanufaisha wanachama, na vinaendeshwa kwa uadilifu mkubwa,” amesema Chongolo.

Katika hatua nyingine, serikali imeweka mkazo katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali ili kurahisisha ufuatiliaji wa shughuli za kifedha, kuongeza uwazi, na kubaini mapema viashiria vya ubadhirifu.

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa juhudi hizo zinatekelezwa kupitia kampeni maalum ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” inayolenga kuimarisha utawala bora ndani ya vyama vya ushirika.

Amefafanua kuwa kampeni hiyo itadumu kwa miaka mitatu na itakuwa ikifanyiwa tathmini kila mwaka ili kupima mafanikio, kubaini changamoto, na kuweka mikakati ya maboresho zaidi.

Aidha, kampeni hiyo itahusisha ukaguzi wa mara kwa mara, utoaji wa elimu kwa wanachama, pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya kupokea taarifa kutoka kwa wadau na watoa taarifa (whistleblowers) ili kusaidia kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu.

Pia, serikali inapanga kuanzisha maafisa uadilifu (integrity officers) ndani ya vyama vya ushirika ili kuongeza uwazi, kuimarisha nidhamu ya kifedha, na kujenga imani ya wanachama kwa viongozi wao.

Serikali inaamini kuwa kupitia mkakati huo mpya, vyama vya ushirika vitaimarika zaidi, vitaongeza tija kwa wanachama wake, na kuwa chachu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.











Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.