MRADI WA ESP KUNUFAISHA WASICHANA ZAIDI YA 60 NZEGA.
Na Allan Kitwe, Tabora.
WASICHANA zaidi ya 60 wanaotoka katika familia zisizo na uwezo Wilayani Nzega Mkoani Tabora wanatarajiwa kunufaika na mradi wa uwezeshaji mtoto wa kike kupata ujuzi (Empowerment Through Skills Program in Tanzania-ESP).
Mradi huo unaofadhiliwa na nchi ya Canada (Canada Fund) kwa lengo la kuwezesha watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu kupata fursa za ujuzi, unatekelezwa katika Vyuo 12 viivyopo katika Mikoa zaidi ya 8 hapa nchini.
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Mwanhala, Nzega ni miongoni mwa vyuo 12 vilivyoingizwa katika program ya ufadhili ili kutoa mafunzo hayo ya muda mfupi (short course) kwa watoto wa kike.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Chuo hicho Enock Lalida, Afisa Utumishi Hekima Amri Lupembe ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu sana kwa kuwa unawapa fursa watoto wa kike kupata ujuzi.
‘Wasichana 30 wanaotoka katika kaya zinazoishi katika mazingira magumu Wilayani hapa tayari wamesajiliwa na kuanza mafunzo ya kozi fupi za fani mbalimbali ili waweze kujikwamua kimaisha, kundi lingine litafuata’, amesema.
Ametaja baadhi ya fani wanazojifunza kuwa ni ushonaji na ubunifu wa mavazi, umeme wa majumbani, uungaji vyuma, ujenzi (uashi) na ufundi bomba, mafunzo hayo hutolewa kwa kipindi cha miezi sita sita.
Mmoja wa wasichana waliopata fursa hiyo, Judith Kulinge (25) kutoka Kijiji cha Puge Wilayani humo ameishukuru serikali ya Canada na Tanzania kwa kutoa fursa za mafunzo hayo kwa watoto wa kike wanaotoka katika kaya zisizo na uwezo.
Akielezea mafanikio ya Chuo hicho, Afisa Utumishi ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya chuo hicho na kuwapatia vifaa vya kutosha vya kujifunzia na kufundishia katika kozi mbalimbali.
Ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoka Wilaya na Mikoa yote nchini kuleta watoto wao ili wapate mafunzo bora ya ufundi ili waweze kuajiriwa au kujiajiri.




Maoni