MKENDA:URASIMISHAJI UJUZI KUINUA HADHI YA VIJANA
Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema programu ya utambuzi na urasimishaji ujuzi inalenga kumpa kijana hadhi, sauti na fursa pana za ajira ndani na nje ya nchi.
Amesema hayo Aprili 22, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi, inayolenga kuwasaidia vijana wenye ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi kutambuliwa kitaaluma.
“Ujuzi ni mali, mtaji na nguvu ya taifa, hivyo vijana wanapaswa kujitokeza ili kutathminiwa na kurasimishwa,” amesema.
Ameeleza kuwa utoaji wa vyeti kupitia programu hiyo siyo tu utoaji wa nyaraka, bali ni njia ya kumpa kijana nafasi ya kushindana katika soko la ajira kwa kuaminika zaidi.
Aidha, amesema serikali imepanga kusogeza huduma karibu na wananchi ili mafundi wasilazimike kusafiri umbali mrefu, huku akisisitiza kuwa mchakato huo unatekelezwa bila gharama kwa wanufaika.
Ameongeza kuwa si kila mwenye ujuzi atapewa cheti moja kwa moja, bali watafanyiwa tathmini, na wale watakaobainika kuwa na mapungufu watapatiwa mafunzo ya ziada ili kufikia viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amesema lengo ni kuwafikia wananchi 80,000 ifikapo mwaka 2027.
Amebainisha kuwa kwa mwaka huu serikali imelenga kuwafikia watu 30,000, ambapo tayari fedha zimetolewa kuwafikia wananchi 14,400 bila malipo.
Amesema serikali imetenga takribani shilingi milioni 600 kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo, ambayo pia inalenga kuongeza ajira na fursa mbalimbali kwa wananchi watakaonufaika na vyeti vinavyotambulika rasmi.



Maoni