MATAPELI WATANO WANASWA KWA TUHUMA ZA KUIBA MILIONI 40 TABORA
Na mwandishi wetu, Tabora.
Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa shilingi milioni 40 kutoka kwa mfanyabiashara Fatuma Nasoro, mkazi wa Wilaya ya Kaliua, katika tukio lililotikisa wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, watuhumiwa hao walinaswa kufuatia msako maalum ulioendeshwa kwa nyakati tofauti ndani ya mkoa huo, baada ya kubainika kuwa walikuwa wakijihusisha na vitendo vya utapeli huku wakiendelea na maisha yao ya kawaida bila wasiwasi wowote.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Matiko Chacha, amesema miongoni mwa waliokamatwa, wawili wanaotambulika kwa majina ya Marseli Gwasima na Fred Ricardo walitumia mbinu za udanganyifu kwa kujifanya wahudumu wa kampuni ya mawasiliano ya YAS (zamani Tigo).
Ameeleza kuwa kwa kutumia ujanja huo, watuhumiwa walimshawishi mfanyabiashara huyo, anayejihusisha na biashara ya khanga na vitenge wilayani Kaliua, kuwasajili laini yake, hatua iliyowapa mwanya wa kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti yake ya benki na kuzipeleka kwenye namba zao za simu.
Katika msisitizo wake, Mkuu huyo wa Mkoa ameonya kuwa serikali haina uvumilivu kwa vitendo vya uhalifu, akibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na matukio kama hayo.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuwa makini wanapopokea huduma kutoka kwa watu wanaojitambulisha kama mawakala au wahudumu wa kampuni za mawasiliano, na kuhakikisha wanathibitisha uhalali wao ili kuepuka kuingia kwenye mitego ya matapeli.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, akieleza kuwa wanaendelea kushikiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wake, Fatuma Nasoro ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Tabora kwa juhudi zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, akisisitiza kuwa hatua kali zichukuliwe ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na vitendo vya utapeli.



Maoni