LISHE BORA SHULENI YATAJWA KUWA MSINGI WA MAFANIKIO YA ELIMU

 


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

KAMISHINA wa Elimu Tanzania, Dk Lyabwene Mtahabwa, amesema mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji hauwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa huduma bora za chakula na lishe shuleni.

Amesisitiza kuwa wadhibiti ubora katika halmashauri zote wanapaswa kuhakikisha chakula kinachotolewa kwa wanafunzi kinazingatia viwango vya ubora ili kuepusha madhara ya kiafya ikiwemo viriba tumbo.

Dk Mtahabwa alitoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mradi wa CRISP unaotekelezwa na SwissAid kwa miaka mitatu katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam.

Amesema maboresho ya elimu hayawezi kuleta matokeo chanya kama hayatazingatia lishe ya wanafunzi, akibainisha kuwa serikali imeweka sera na miongozo kuhakikisha shule zinatoa huduma ya chakula.

“Mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji hatuwezi kufanikiwa bila kuwa na huduma bora za chakula na lishe,” amesema Dk Mtahabwa.

Ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali kuimarisha lishe shuleni, ikiwemo waraka wa mwaka 2006 uliolenga kushirikisha jamii pamoja na mwongozo wa utoaji wa chakula mashuleni uliotolewa mwaka 2020 na kuzinduliwa 2021.

Aidha, amesema mwaka 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alisaini mkataba wa lishe na wakuu wa mikoa ili kuboresha huduma za chakula shuleni kote nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa SwissAid Tanzania, Betty Malaki, amesema mradi wa CRISP utasaidia wanafunzi kupata lishe bora huku ukiwapatia wakulima soko la uhakika.

Naye Ofisa Programu wa Sera kutoka World Food Programme, Abiud Gamba, amesema lishe shuleni huongeza mahudhurio, umakini na ufaulu wa wanafunzi darasani.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa lishe kamili, hususan vyakula vya protini, mboga na matunda, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano ili kuboresha afya na maendeleo ya wanafunzi.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.