KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YASISITIZA UFANISI WA MIRADI YA MAENDELEO YA SEKTA YA MADINI

 



Na Hamida Ramadhan, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Serikali kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi yote ya sekta ya madini ili kuhakikisha inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa taifa.

Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo bungeni Aprili 27, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Simon Lusengekile, alisema Serikali inapaswa kuhakikisha miradi ya maendeleo inapatiwa rasilimali za kutosha pamoja na usimamizi madhubuti ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Alibainisha kuwa usimamizi imara wa miradi hiyo utaongeza tija katika sekta ya madini na kuboresha huduma kwa wananchi kupitia miradi ya kimkakati inayolenga kuongeza thamani ya rasilimali za madini.

Kamati imeishauri Wizara kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia mipango ya taifa, viwango vya ubora na muda uliopangwa ili kuepuka ucheleweshaji na kupunguza changamoto za utekelezaji.

Aidha, imeitaka Serikali kuimarisha usimamizi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake kwa weledi na uwajibikaji.

Katika hatua nyingine, Kamati imependekeza kuwekeza zaidi kwenye teknolojia za kisasa za uchenjuaji wa madini ili kuongeza thamani ya rasilimali kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Pia, imehimiza ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa sekta ya madini ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.