HAWA MWAIFUNGA AAHIDI TABASAMU KWA WAKAZI MANISPAA TABORA
Na Allan Kitwe, Tabora.
MBUNGE wa Jimbo la Tabora Mjini Hawa Subira Mwaifunga amefanya mkutano mkubwa wa hadhara Jimboni humo na kupokea kero za wananchi huku akiahidi kuwapa tabasamu kwa mazuri yatakayofanyika.
Ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika uwanja wa TBC ulio karibu na Ofisi za CCM Tabora Mjini ambapo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi na wana CCM wote kwa kumchagua kuwa mbunge wao.
Mwaifunga amesema kuwa kuanzia sasa ataanza utaratibu wa kupita mtaa kwa mtaa, kata kwa kata ili kupokea mawazo ya nini wananchi wanataka, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Amefafanua kuwa mbunge ni mtumishi wa wananchi, hivyo ana wajibu wa kutembelea, kusikiliza na kutatua kero na shida za wananchi wake kwa kuwa ndio waliompeleka bungeni.
‘Mbunge na diwani wanawajibika moja kwa moja kwa waliowachagua, kwa kuhakikisha wanajua kero zao na kuzitafutia ufumbuzi, kazi yetu ni kuwapa tabasamu wananchi na si vinginevyo,’ ameeleza.
Wananchi wanataka kuona mambo mazuri, wasipoona kinachofanyika au kuwatembelea ili kujua changamoto zao hawawezi kukuelewa, wanachotaka ni kuona kiongozi wao akiwajibika katika mambo yao.
Mwaifunga amesisitiza kuwa yale yote aliyoyaahidi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana atahakikisha yanatekelezwa kwa vitendo ili kuleta tabasamu kwa wapiga kura wake.
‘Nawashukuru sana kwa kura nyingi mlizonipa na ushirikiano mkubwa mnaoendelea kunipatia tangu nimeingia bungeni kama mwakilishi wenu, Ofisi yangu iko wazi masaa 24 kwa ajili yenu, kama sipo, Katibu wangu yupo’, alisema.
Ndani ya siku 100 za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hadi sasa kazi kubwa imefanyika katika Jimbo hili na kuahidi kuwa mambo mazuri yanakuja ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo kuendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa.
Katika mkutano huo, mbunge amepokea na kutolea ufafanua kero mbalimbali za wananchi kupitia wakuu wa idara wa halmashauri ya manispaa Tabora na nyingine alizichukua na kuahidi kuziwasilisha bungeni.
Awali akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete amewashukuru wananchi kwa kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi na kuahidi kuwa chama hakitawaangusha, kitawaletea maendeleo.

Maoni