ENABEL YAWEZESHA MABINTI 200 KASULU KUPATA ELIMU

 



Na Allan Kitwe, Kasulu. 

SHIRIKA la Maendeleo la Ubelegiji (ENABEL) limeunga mkono juhudi za serikali kwa kuwezesha watoto wa kike zaidi ya 200 Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kupata mafunzo ya ujuzi katika Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu (FDC).

Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Chuo hicho Fridegarda Mukyanuzi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake ambapo ameeleza kufurahishwa na ujio wa mradi huo ili kuwezesha wasichana wasio na uwezo.

Amebainisha kuwa kupitia mradi huo Shirika limegharamia mahitaji yote ya Chuo kwa watoto hao na kuwawezesha kusoma fani mbalimbali za ufundi ikiwemo ushonaji nguo, ususi na urembo, umeme wa majumbani na ufundi bomba.

Fani nyingine ni ufundi magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, umeme wa magari na wa majumbani na kila wanapohitimu Shirika huwawezesha vifaa vya kuanzia shughuli zao.

Amefafanua kuwa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 umekuwa mkombozi kwa Chuo na kwa watoto hao kwani umesaidia kuboresha mazingira na miundombinu ya chuo kwa ujumla.

Mradi huu umewajengea uwezo wa kiufundi na ujasiriamali, hata wanapohitimu na kurudi nyumbani wanakuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao, baadhi wanaajiriwa na wengine huamua kuanzisha shughuli zao za kuwaingizia kipato.

Kupitia programu hii, Shirika limeunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwapatia ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

'Lengo la mradi huu ni kuwezesha wasichana wanaotoka katika familia duni waweze kumudu maisha, kwa kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi ili waweze kutimiza ndoto zao na kuwa msaada kwa familia zao', amesema.

Kupitia mradi huo amefafanua kuwa jumla ya wasichana 209 wameshanufaika na mafunzo mbalimbali, pia umewezesha kujengwa Kituo cha Jinsia, ukarabati wa karakana, vifaa vya mafunzo na ujenzi wa eneo la michezo ya watoto.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.