DC MYINGA ATOA AGIZO ZITO KWA VIONGOZI SIKONGE JUU YA UPUNGUFU WA MADAWATI KWA SHULE ZA MSINGI.




Na Mwandishi Wetu, Sikonge-Tabora. 

UPUNGUFU wa madawati katika shule za msingi Wilayani Sikonge umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Thomas Myinga, kutoa agizo kali kwa viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanatumia rasilimali zilizopo kumaliza changamoto hiyo kwa haraka.

Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji, kata pamoja na walimu, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mheshimiwa Myinga alisisitiza kuwa hakuna sababu ya wanafunzi kuendelea kukaa chini ilhali maeneo yao yana rasilimali za kutosha, ikiwemo misitu inayoweza kutumika kutengeneza madawati.

Alielekeza viongozi hao kupanga na kutekeleza bajeti zao kwa kuzingatia kipaumbele cha elimu, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya serikali, wananchi na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Seif Salum, aliweka wazi ukubwa wa tatizo hilo kwa kutoa takwimu za madawati yaliyopo na upungufu uliopo katika shule mbalimbali za msingi wilayani humo, akisisitiza umuhimu wa hatua za haraka kuchukuliwa.

Katika mjadala wa kikao hicho, baadhi ya viongozi na wadau walipendekeza serikali kuvikabidhi vijiji magogo yaliyokatwa ili yaweze kutumika kuchonga madawati, hatua ambayo walieleza itarahisisha upatikanaji wa samani hizo muhimu kwa gharama nafuu. Wadau hao pia waliahidi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha agizo la Mkuu wa Wilaya linatekelezwa kwa wakati.

Naye Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Sikonge, Richard Mwita, aliwataka viongozi kusimamia kikamilifu fedha zitakazochangwa na wadau pamoja na kuweka takwimu sahihi, ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Hatua hiyo inaonekana kuibua matumaini mapya kwa wanafunzi wa Wilaya ya Sikonge, huku jamii ikihimizwa kushiriki kikamilifu katika kuboresha sekta ya elimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.










Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.