CCM YATAKA WATENDAJI, WATAALAMU KUWAJIBIKA IPASAVYO
Na Gilbert Dioniz na Allan Kitwe, Ngara
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Ngara Mkoani Kagera kimewataka Watendaji na Wataalamu waliopewa dhamana kusimamia miradi ya maendeleo kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngara Vitalice Ndairagije kwenye ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya kukagua miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa kiu ya wananchi ni kuona miradi inayotekelezwa na serikali yao inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, na hili haliwezi kufanikiwa kama Watendaji na Wataalamu waliopewa dhamana hawatafanya kazi kwa weledi.
‘Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuleta mamilioni ya fedha hapa Ngara kwa ajili ya miradi ya maendeleo, fedha hizi tunataka zifanye kazi iliyokusudiwa na zisimamiwe ipasavyo’, amesema.
Mwenyekiti alidokeza kuwa miradi ikisimamiwa ipasavyo itakamilika kwa wakati na thamani ya fedha zilizotumika itaonekana, hivyo akaagiza Wakuu wa Idara kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi yote inayotekelezwa katika idara zao.
Kila Mkuu wa idara akifanya kazi kwa weledi na kutanguliza uzalendo katika majukumu yake hakuna mradi utakaotekelezwa chini ya kiwango na wananchi wataendelea kuiamini serikali yao na Chama Cha Mapinduzi.
Ndairagije ameeleza kuwa anatamani miradi inayotekelezwa katika Wilaya hiyo iwe mfano kwa wilaya zingine hasa kutokana na ubora wake na kukamilika kwa wakati ili kunufaisha wananchi.
Naye Katibu wa Chama wa Wilaya hiyo Mariam Amiry amebainisha wazi kuwa wananchi wanaipenda sana serikali yao ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa inawajali na kuwaletea maendeleo kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa.
Amesisitiza dhamira ya serikali ya CCM kuwa ni kuinua uchumi wa wananchi kutoka uchumi wa chini hadi wa kati ambao kiini chake ni miundo mbinu safi na ya kuvutia, ili jamii ipate huduma bora.
Mkuu wa wilaya hiyo Kanali Mathias Kahabi amewataka watendaji wa idara zote kusimamia vyema miradi hiyo huku akimtaka Meneja wa RUWASA Wilaya kuhakikisha mradi wa maji wa Kumubuga unakamilika haraka ili kumaliza kero iliyopo sasa.
Amefafanua kuwa miradi mingi inayotekelezwa katika Wilaya hiyo iko vizuri ila akamtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuchukua hatua stahiki kwa wakuu wa idara wasiotimiza wajibu wao ipasavyo.


Maoni