ASKOFU MEIVUKIE AASA JAMII KUCHUKUA TAHADHARI
Na Allan Kitwe, Tabora
WAKRISTO na jamii kwa ujumla wameaswa kuchukua tahadhari na kumwomba Mungu ainue wapatanishi dhidi ya mataifa ya Marekani, Israel na Iran ili vita inayoendelea sasa baina yao imalizike kwa amani ili kuepusha athari kwa jamii.
Wito huo umetolewa jana na Askofu Paul Meivukie wa Kanisa la TAG-Jimbo la Tabora Kati ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kitete Christian Centre (KCC) alipokuwa akitoa salamu za pasaka kwenye ibada kanisani hapo.
Amesema kuwa athari za vita vinavyoendelea sasa katika mataifa hayo ni kubwa mno, na Tanzania sio kisiwa, haiwezi kujitegemea kwa kila kitu, hivyo ni muhimu sana kumwomba Mungu na kutumia vizuri chakula tulicho nacho.
Huu sio wakati wa kulaumu viongozi bali kuwaombea ili Mwenyezi Mungu awaongoze na kuwapa hekima ya kutoa maamuzi sahihi ili kuepusha bei za bidhaa kupanda zaidi hali inayoweza kuleta shida kwa wananchi.
‘Sote tunafahamu vita inayoendelea baina ya Marekani, Israel na Iran, naomba tuendelee kuchukua tahadhari, petroli inavyoendelea kupanda vitu vingine vitapanda pia, tutumie kwa uangalifu mkubwa chakula tulicho nacho,’ ameongeza.
Akinukuu maandiko kutoka kitabu cha Wagalatia 4: 5 Askofu Meivukie ameasa waumini wa kanisa hilo na jamii kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa amani, upendo, umoja, mshikamano na hekima kwa viongozi waliopewa dhamana.
Aidha amewataka kuendelea kuishi kama wana wa Mungu, kumtumaini katika kila jambo na kuombeana ili makusudi yake yatimizwe katika maisha yao na taifa kwa ujumla na lolote lililo kinyume na mapenzi yake lisipate nafasi.
Akihitimisha Semina ya siku 5 ya Pasaka katika ibada hiyo, Askofu Julius Tibuhinda wa Kanisa la TAG Biharamulo amewataka waumini wa Kanisa hilo kuheshimu ibada, maombi na kukubali kuongozwa na Roho wa Mungu.
Amedokeza kuwa kanisa la kwanza lilipata mafanikio makubwa kwa sababu liliishi misingi ya Yesu Kristo, ambayo ni kudumu hekaluni mwa Bwana, kumwomba Mungu na kuongozwa na Roho Mtakatifu.






Maoni