ZAIDI YA WATOTO 173,255 IGUNGA KUPATIWA CHANJO YA POLIO BAADA YA KIRUSI KUGUNDULIKA JIJINI MWANZA

 


Na Lubango Mleka, Igunga. 

Zaidi ya watoto 173,255 wenye umri chini ya miaka kumi wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa polio wilayani Igunga mkoani Tabora, kufuatia kugundulika kwa kirusi cha ugonjwa huo mkoani Mwanza.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo hatari, hasa kwa watoto wadogo ambao wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi.

Katika kujiandaa na zoezi hilo, Hospitali ya Wilaya ya Igunga imetoa elimu kwa wadau wa afya kwa lengo la kuwajengea uelewa pamoja na kuongeza nguvu ya uhamasishaji kwa jamii ili kuhakikisha mwitikio unakuwa mkubwa wakati wa utekelezaji wa chanjo hiyo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Chanjo wilayani Igunga, Novat Bijana, pamoja na wataalam wengine wa afya, walisisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto kupata chanjo ili kujikinga na madhara ya ugonjwa wa polio.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Igunga, Bi. Elizabeth Rwegasila, aliwataka wadau hao kufikisha elimu waliyoipata kwa jamii na kuwatoa hofu wananchi kuhusu usalama wa chanjo hiyo.

Wadau wa afya wakiwemo viongozi wa dini wilayani humo wameahidi kuwa mabalozi wa uhamasishaji kwa jamii, wakisisitiza kuachana na imani potofu kuhusu chanjo na badala yake kushirikiana na wataalam wa afya watakapofika katika maeneo yao.

Baadhi yao, akiwemo mchungaji wa Kanisa la KKKT Naonawelu Abelshuu pamoja na Katibu wa BAKWATA Igunga, Alhaj Juma Mihambo, wameitaka jamii kuwa tayari kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu la afya ya umma.

Kwa mujibu wa serikali, zoezi la utoaji chanjo ya polio linatarajiwa kufanyika katika mikoa saba ambayo ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Geita, Mara na Singida, ikiwa ni hatua ya tahadhari dhidi ya kusambaa kwa ugonjwa huo nchini.















Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.