WAKULIMA TABORA WANUFAIKA NA MNADA WA KWANZA WA KOROSHO
Na Lubango Mleka, Tabora.
WAKULIMA wa zao la korosho mkoani Tabora wameanza kunufaika na fursa ya soko baada ya kuanza kwa mnada wa kwanza wa zao hilo, ambapo zaidi ya kilo elfu kumi na tatu zimeuzwa katika siku ya ufunguzi.
Mafanikio hayo yameelezwa kuwa ni ishara ya kukua kwa zao la korosho mkoani humo, huku matarajio ya awali yakiwa ni kuuza kilo elfu kumi pekee. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shabani Katalambula, amesema mwitikio wa wakulima ni mkubwa na unaonyesha wazi kuwa zao hilo linaweza kuwa tegemeo jipya la kiuchumi kwa wakazi wa Tabora.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa kampuni ya Mateak Holdings Ltd, Violet Mordichai, amesema wamejikita katika kuwajengea uwezo wakulima kupitia elimu ya kilimo bora cha korosho, akisisitiza matumizi ya pembejeo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora , Bi Upendo Wella, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, amewataka wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili kuwa na nguvu ya pamoja katika uzalishaji na uuzaji wa korosho, pamoja na kupata masoko yenye uhakika.
Baadhi ya wakulima walioshiriki mnada huo wameeleza kufurahishwa na bei waliyouza mazao yao, wakihimiza wenzao kutumia mapato hayo kuboresha maisha ya familia, ikiwemo kuwekeza katika elimu ya watoto.
#Habarimaelezo #habarikamilitv #RCPaulChacha #koroshotabora #halmashauriyaUyui








Maoni