TANROADS YAPELEKA TABASAMU MWAMGONGO
Na Allan Kitwe, Kigoma.
WAKAZI wa Kitongoji cha Mgazo, Mtaa wa Lubona katika Kijiji cha Mwamgongo Kata ya Mwamgongo Wilaya ya Kigoma wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuanza kufungua barabara inayoingia kijijini kwao.
Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari jana wameeleza kuwa tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 Kijiji hicho hakijui usafiri wa barabara kwa sababu kiko kwenye milima na usafiri pekee wanaotegemea ni wa mitumbwi na boti.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lubona, Elias Lutaha ameeleza kufurahishwa na hatua ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuipatia TANROADS Kigoma shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kuchonga milima na kuanza kufungua barabara hiyo.
‘Tangu tumepata uhuru barabara hii indo imeanza kufunguliwa, kwa sasa ukitoka Kigoma Mjini kupitia Mkongoro unafika katika Kitongoji hiki kwa usafiri wa barabara lakini haifiki Mwamgongo Kijijini’, ameeleza.
‘Barabara yetu imefunguliwa kutoka Chankere hadi hapa Mganzo lakini haifiki Mwamgongo, chonde chonde, Mheshimiwa Rais, tunaomba utusaidie ili barabara hii ifike Mwamgongo hadi Kagunga ili kumaliza kero yetu’, ameomba.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma Mhandisi Charo Kimata ameishukuru Serikali kwa kuwapatia kiasi hicho cha fedha kwani kimesaidia kufungua km 11 za barabara hiyo na tayari imeanza kutumika.
Amefafanua kuwa kutokana na milima hiyo kuwa na mawe mengi na miteremko mikali baadhi ya maeneo wamejenga barabara ya zege na changarawe, na watakapopata fedha nyingine wataendelea kufungua barabara hiyo hadi mwisho.
Mhandisi Kimata amedokeza kuwa wakazi wa Vijiji vya Mwamgongo na Kagunga wanapata adha kubwa ya usafiri kwa kuwa usafiri pekee wanaotumia ni wa boti na mitumbwi ndani ya ziwa Tanganyika, magari hayafiki huko hadi wapitie nchi jirani ya Burundi.
Amebainisha kuwa wameshaomba kiasi kingine cha shilingi bilioni 5 ili kuendelea kufungua barabara hiyo hadi kufika Makao Makuu ya Kata, Mwamgongo na baadae wataendelea hadi Kagunga.





Maoni