TAFITI ZAENDELEA KUTUMIKA KATIKA MAAMUZI YA SERA KUPITIA PORTAL MPYA YA SERIKALI
Na Jasmine Shamwepu,Dodoma
HATUA ya Serikali kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kusambaza tafiti mbalimbali nchini, inatarajiwa kuleta mapinduzi katika matumizi ya ushahidi wa kisayansi kwenye maamuzi ya sera na mipango ya maendeleo.
Kupitia portal hiyo mpya, matokeo ya tafiti yaliyokuwa yakibaki kwenye makabrasha au kuhifadhiwa ndani ya taasisi, sasa yatapatikana kwa urahisi na kutumiwa moja kwa moja na watunga sera, wataalamu pamoja na wadau wa maendeleo.
Akizungumza Machi 23, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa wa taasisi za utafiti, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, amesema mfumo huo ni sehemu ya mageuzi ya kimkakati ya kuifanya Tanzania kuwa taifa linaloongozwa na ushahidi katika kufanya maamuzi.
Ameeleza kuwa portal hiyo itaongeza uwazi, kuimarisha ushirikishwaji wa wadau na kuhakikisha tafiti zinatumika kutatua changamoto halisi za wananchi.
“Mfumo huu utasaidia kuunganisha watafiti na watunga sera ili kuhakikisha tafiti zinakuwa na mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya taifa,” amesema.
Aidha, Dkt. Kida amesisitiza kuwa mpango huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursali Milanzi, amesema Tume ya Taifa ya Mipango itaendelea kusimamia mwelekeo wa uchumi kwa kuchambua masuala muhimu kama mfumuko wa bei, mapato na matumizi ya Serikali pamoja na kuhakikisha ukuaji endelevu.
Ameongeza kuwa uratibu wa mipango ya maendeleo katika ngazi zote utaimarishwa ili kuhakikisha utekelezaji wake unaendana na malengo ya taifa.
Mkutano huo wa siku mbili umezikutanisha taasisi za utafiti na Serikali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinajibu mahitaji ya maendeleo ya nchi.
Kwa ujumla, uzinduzi wa portal hiyo unaashiria hatua mpya kwa Tanzania katika kutumia tafiti kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.



Maoni